0



JESHI la Polisi jana limeanza kufanya ukaguzi wa leseni na vyeti vya madereva kwenye Kituo Kikuu cha Mabasi ya Mikoani na nchi jirani Ubungo
(UBT), jijini Dar es Salaam kufuatia ajali za barabarani nchini kuongezeka.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga,
alisema kuwa ukaguzi huo una lengo la
kuchunguza madereva ambao wanafanya shughuli
hizo kinyume na sheria na kusababisha kuwapo kwa ajali nyingi za barabarani.
“Lengo letu ni kuhakikisha madereva wanakuwa na vyeti pamoja na leseni halali. 

Hakuna atakayeachwa katika zoezi hili kwa sababu linaendeshwa katika mikoa yote ambayo mabasi makubwa yanasafiri ili kuepusha ubabaishaji wa
madereva,” alisema.
Kuhusu malalamiko ya kuwapo urasimu katika zoezi hilo, Kamanda Mpinga alisema hata kama
dereva hatakaguliwa katika kituo cha Ubungo, atakwenda kukaguliwa mikoani ili kufanikisha zoezi hilo.

Umoja wa Madereva wa Mabasi (UWAMATA), ulilalamikia kuwapo kwa urasimu katika zoezi hilo
kwa madai kuwa madereva wengi hawajakaguliwa.

Mmoja wa wajumbe wa umoja huo, Jabu
Chagenya, alisema serikali inapaswa kuwa na nia ya dhati katika kupambana na tatizo hilo na kuacha kutimiza majukumu yake kisiasa.
“Huwezi kufanya ukaguzi wa aina hii kwa kuuliza namba ya leseni pamoja na kuhoji cheti, ingepaswa kuwapo kwa ushirikishwaji wa Chuo
cha Taifa cha Usafirishaji na Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi ili kutambua vyeti hivyo kama ni feki.

“Kilichotokea ni usumbufu kwa abiria na kama wataendelea kufanya ukaguzi kwa mtindo huu sidhani kama utakuwa na mafanikio kwa kuwa
watu ambao tunajua matatizo ya madereva hatushirikishwi,” alisema Chagenya.


Credit: Mtanzania

Chapisha Maoni

 
Top