HOSPITALI ya Serikali mkoani Shinyanga juzi ilijikuta katika wakati mgumu baada ya kundi la wananchi kuvamia wodi ya wazazi, wakilalamikia
uzembe uliofanywa na muuguzi kushindwa kutoa msaada kwa mwanamke aliyekuwa akijifungua na
kusababisha kifo chake na watoto wake mapacha aliokuwa anajifungua.
Hali hiyo ilijitokeza saa 12 juzi jioni baada ya wazazi wa mjamzito huyo aliyekuwa akijifungua kulalamikia kitendo cha muuguzi aliyekuwa zamu
katika wodi hiyo kutomsaidia binti yao mwenye umri wa miaka 15.
Kutojali kwa muuguzi huyo ndiko kunadaiwa kusababisha vifo vya watoto mapacha hao wawili na mama yao.
Muuguzi huyo anadaiwa kushindwa kumhudumia mjamzito huyo hata pale alipobembelezwa na wazazi wa mjamzito huyo, lakini yeye aliendelea
kushughulika na simu yake ya kiganjani, akidaiwa kuwasiliana na watu wengine.
Kwa mujibu wa wazazi wa marehemu huyo, muuguzi huyo aliwajibu kuwa atamshughulikia baadae kwani alishamuona. Baada ya wananchi kupata taarifa hizo waliingia wodini kwa hasira.
Akizungumza kwa uchungu na waandishi wa habari, mama mzazi wa binti aliyejifungua, Mwanahamisi Juma, mkazi wa Mshikamano Manispaa ya Shinyanga, alisema awali binti yao
alipelekwa Zahanati ya Kambarage kwa ajili ya kujifungua.
Baadaye alihamishiwa Hospitali ya Mkoa baada ya kubainika kuwa na tatizo. Mwanahamisi alisema baada ya kufikishwa hospitalini hapo saa sita
mchana na kupokelewa na wauguzi ilipofika saa 10 jioni alishikwa na uchungu wa kujifungua na aliomba msaada kwa muuguzi aliyekuwa zamu
ambaye hata hivyo hakumjali na badala yake aliendelea kuongea na simu yake ya kiganjani.
"Huyu muuguzi alitushangaza maana pamoja na mtoto wetu kuomba msaada ili asaidiwe aweze kujifungua salama, yeye hakuonesha kujali kabisa,
aliendelea na shughuli zake za kuchati na simu yake ya mkononi, hali iliyotulazimisha tumfuate na kumlalamikia, hata hivyo alisema tumuache maana mzazi alikuwa akiendelea kusukuma," alisema na kuongeza;
"Tulilalamika sana na hata baadhi ya wananchi wengine walikuja kutusaidia kumuomba muuguzi huyo amsaidie, lakini hakujihangaisha kabisa,
hivyo tulitafuta msaada wa muuguzi mwingine aliyekuwa jirani ili amsaidie binti yetu, alifika na kutoa msaada hata hivyo watoto wote walikuwa
wameishakufa," alieleza Mwanahamisi.
"Saa 10 mwanangu alianza kusukuma na kujifungua mtoto wa kwanza wa kike, lakini tayari alikuwa amefariki na muda mfupi baadaye alijifungua mtoto mwingine wa pili wa kiume naye hakuchukua muda pia, alifariki, kwa kweli tulisikitishwa sana na kitendo cha muuguzi huyo," alisema Mwanahamisi.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Gibson Robert, mkazi wa mjini Shinyanga alielezea kushangazwa kwake na kitendo cha muuguzi
huyo kushindwa kutoa huduma kwa mjamzito huyo na kusababisha vifo vya mapacha hao wawili na mama yao.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Fredrick Mlekwa, akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa alikanusha
vifo vya mapacha hao kusababishwa na uzembe wa muuguzi na kwamba mimba hiyo ilikuwa haijatimiza muda wake wa miezi tisa hivyo kitaalam watoto hao wasingeweza kuishi kwa vile
hawajakamilika.
"Ni kweli jana (juzi) palitokea tatizo katika hospitali yetu baada ya wananchi kuvamia wodi namba nane ambayo ni ya wazazi wakilalamikia kitendo cha muuguzi kushindwa kumsaidia
mwanamke mmoja aliyekuwa akijifungua na kusababisha vifo vya watoto waliozaliwa," alisema
Dkt. Mlekwa na kuongeza;
"Binafsi baada ya kupata taarifa hizo nilikwenda katika wodi hiyo na tulipofuatilia tulibaini kuwa
mimba ya mjamzito huyo ilikuwa haijafikisha umri wa kujifungua kwani ilikuwa na umri wa miezi
sita... mzazi mwenyewe alikiri muda huo na kitaalamu isingekuwa rahisi kwa watoto hao kuishi," alifafanua Dkt. Mlekwa.
Dkt. Mlekwa aliendelea kufafanua kuwa pamoja na maelezo ya mzazi mwenyewe kukiri umri wa ujauzito wake (miezi sita) walichunguza miili ya
watoto waliozaliwa na kuipima ambapo mmoja alikuwa na uzito wa gramu 500 na mwingine gramu 700, hivyo kitaalamu walikuwa hawajakamilika kuitwa binadamu.
"Ni kweli tumefuatilia kuhusu suala la muuguzi wa zamu kuongea na simu, tumemuhoji amekiri muda huo alikuwa akiongea na simu na kufafanua
kuwa alikuwa akiwasiliana na daktari wa zamu kwa ajili ya kuomba msaada zaidi wa kumsaidia mzazi huyo," alisema na kuongeza kwamba suala hilo watazidi kulichunguza.
Dkt. Mlekwa amerejea kutoa wito kwa wakazi wa Shinyanga kuwa na tabia ya kuheshimu taratibu za hospitali zilizopo na kueleza kuwa ni kosa la
kisheria kwa wananchi wa kawaida kuingia ndani ya wodi ya wazazi, hali ambayo inawezabkusababisha maambukizo mbalimbali kwa watoto
wanaozaliwa kwa vile wanakuwa hawapatiwa chanjo za kinga.
Chapisha Maoni