Siku tatu kabla ya Bunge la Katiba kuanza kupigia kura Rasimu ya Katiba inayopendekezwa, watu wasiojulikana wameanza kusambaza vitisho vya
kuwatia hofu wajumbe wa Bunge hilo.
Watu hao wamesambaza vipeperushi katika maeneo mbalimbali ya mji wa Dodoma usiku wa kuamkia jana, wakiwataka wajumbe kutoingia
bungeni vinginevyo yatakayowapata watajuta, huku wajumbe kutoka Zanzibar wakitishiwa kwa
ujumbe wa simu kupitia mtandao wa WhatsApp.
Tayari, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd ametoa kauli kuhusu vitisho hivyo akisema Serikali itachukua kila hatua kuhakikisha wajumbe kutoka visiwani humo
ambao wamekuwa wakipokea vitisho wanakuwa salama.
Mbali na kusambazwa kwa karatasi hizo, maandishi mekundu yamechorwa katika kuta za jengo la Makao Makuu ya CCM mjini Dodoma yakisomeka, “No Katiba. No ufisadi.” Vikaratasi vilivyosambazwa vinasomeka: “Onyo.
Dodoma si mahali pa kufuga wezi wa fedha za umma. Utakayeingia bungeni kuanzia kesho (leo), yatakayokupata utajuta.”
Mkazi wa Dodoma, Sospeter Samwel alimwambia mwandishi wetu jana kuwa aliokota baadhi ya vipeperushi hivyo jana saa moja asubuhi katika
eneo maarufu la kuuzia magazeti linalotazamana
na Jengo la CCM.
“Tulikuta hayo makaratasi yametupwa tu
ovyoovyo ila baadaye nikasikia maeneo
mbalimbali mengine nayo yameonekana
yametupwa. Sijui nani hasa watakuwa
wameyasambaza,” alisema.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipoulizwa jana kuhusu na maandishi hayo alijibu
kwa kifupi “No comment” (sina cha kusema).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime jana alitoa taarifa ya maandishi kwa wanahabari akisema jeshi hilo linawasaka watu
waliosambaza vipeperushi hivyo.
“Wananchi na wageni wapenda amani waendelee na shughuli zao kama kawaida kwani polisi tumejiimarisha ipasavyo kukabiliana na yeyote
atakayekiuka sheria na maelekezo yaliyotolewa." Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Rehema Nchimbi
alitoa onyo kwa watu aliodai wanafanya mzaha akisema vyombo vya usalama viko macho saa 24.
Aliwataka wajumbe kutoa taarifa kwa vyombo vya dola wanapoona viashiria vya kutokuwa na usalama.
“Kama ng’ombe mzima tumeshakula tumebakiza mkia tu, niwahakikishie wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, usalama umekuwapo na utaendelea kuwapo."
Wazanzibari kulindwa Akizungumzia vitisho hivyo hasa kwa wajumbe
kutoka Zanzibar, Balozi Idd alisema Serikali itachukua kila hatua kuhakikisha wanakuwa salama.
Alisema kuna ujumbe unazunguka katika mitandao ya jamii ukitoa vitisho kwa wajumbe wa Bunge hilo na watumishi wa sekretarieti ya Bunge
hilo.
“Vyombo vya dola vipo na vitafanya kazi yake. Vinajua vitisho vyote. Niwahakikishie wajumbe mtakuwa salama na Serikali itachukua kila hatua
kuhakikisha hakuna kitakachotokea."
Hoja 17 za Zanzibar Akizungumzia kuhusiana hoja 17 ambazo ziliwasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman zenye masilahi ya visiwa hivyo, Balozi Idd alisema kati yake 13 zilikubalika
na kubakia nne. Hata hivyo, alisema baada ya kuangalia zaidi Rasimu ya Katiba inayopendekezwa waligundua
kuwa zilibakia hoja tatu tu.
Alizitaja hoja hizo kuwa ni ibara 86 ambayo inasema Rais wa Jamhuri ya Muungano atashinda kwa kupata kura zaidi ya asilimia 50. Hata hivyo, alisema waliona kwenye Katiba ya sasa jambo hilo liko kimya kidogo endapo itatokea
mgombea hakupata kura upande wa Zanzibar.
“Tukaona kuwa huyu ni Rais wa Muungano, hivi asilimia 50 yote apate Bara legitimacy (uhalali) yake kama rais wa Muungano iko wapi?” alisema
na kuongeza kuwa vyema katika Rasimu
ikaingizwa kuwa mgombea huyo pamoja na kwamba anatakiwa ashinde kwa zaidi ya asilimia 50, basi angalau katiba iweke kiwango fulani cha kupata upande wa Zanzibar.
Alisema baada ya kutafakari ikakubaliwa Zanzibar angalau mgombea huyo apate asilimia 10 au 15. Hata hivyo, alisema majadiliano kuhusu suala hilo
bado yanaendelea.
Chapisha Maoni