CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema watendaji waliohusika kusababisha mgogoro katika Kiwanda cha Chai Mponde, kilichopo Jimbo
la Bumbuli, Wilaya ya Lushoto, mkoani Tanga, wanapaswa kuwajibishwa pamoja na kuachia ngazi.
Kauli hiyo imetolewa juzi na Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw. Abdulrahman Kinana katika
mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Mponde, Jimbo la Bumbuli, wilayani humo.
Katika mkutano huo, Bw. Kinana alipokea malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya ubabaishaji uliosababisha mgogoro kati ya
wakulima na mwekezaji aliyeuziwa kiwanda hicho kwa madai ya kuwanyanyasa wafanyakazi.
Alisema mgogoro huo umesababisha maisha ya wakulima wa chai wilayani humo kuwa magumu na kushindwa kupeleka watoto shule; hivyo CCM
inataka majibu ya kina juu ya mgogoro huo.
"Hapa Tanzania, kuna tatizo kubwa ambalo limejengeka kwa watendaji wa Serikali kuwa na utamaduni wa kulindana; ndiyo maana wanatengeneza kanuni na sheria nyingi zinazolenga kuwalinda...katika hili chama kinahitaji majibu," alisema.
Alihoji kwa nini jambo hilo limechukua muda mrefu kushughulikiwa, hivyo haliwezi kuishia hivi hivi bila wahusika katika mgogoro huo kuwajibishwa kwani hata Mawaziri, walijiuzulu
kwa sababu ya watu kufa kutokana na Operesheni Tokomeza.
Bw. Kinana alisema wote waliohusika kutoa hati ya kumilikisha kiwanda hicho kwa mwekezaji Yusufu Muller, wawajibishwe kwani sheria zipo
wazi ambapo Ibara ya 13,14, inasema mwekezaji ili aweze kumilikishwa lazima amalize deni.
"Watendaji wengi serikalini wana tabia ya kutengeneza mambo na kulindana...nitakwenda kuzungumza na Rais Jakaya Kikwete, baada ya
mwezi mmoja yaani Oktoba 29 mwaka huu, nitakuja kuwapa jibu, wahusika wanaweza kuwajibika wenyewe," alisema.
Alisema suala hilo lilifika kwa Waziri Mkuu, Bw. mizengo Pinda kutokana na watendaji waliopewa jukumu la kulishughulikia kushindwa kufanya
hivyo ambapo hivi sasa, kuna tabia imeibuka kwa baadhi ya watu kudai Waziri Mkuu anajua migogoro yao kumbe si kweli.
Awali, akitoa taarifa ya mgogoro huo na
kusababisha kufungwa kwa kiwanda hicho, Mbunge wa Bumbuli, Bw. Januari Makamba, alisema wananchi waliingia katika mgogoro na mwekezaji kwa madai ya kuwanyanyasa
wafanyakazi.
"Kiwanda hiki kilikuwa kinamilikiwa na wakulima wenyewe chini ya viongozi wao lakini baadaye, waliingia tamaa ya kukibinafsisha kwa mwekezaji
bila wananchi kupata taarifa.
"Mambo mengine si ya kuzungumza lakini kuna ubabaishaji mkubwa uliofanyika juu ya kiwanda hiki na kusababisha kifungwe, nilifanya juhudi za kuushughulikia mgogoro huu, awali kulikuwa na tatizo la bei ndogo wakulima wanapouza chai
ambayo ni sh. 110 kwa kilo moja nikapambana ikafikia sh. 210," alisema.
Katika mkutano huo, wananchi walimfukuza Diwani wa Kata ya Gunga, Bw. Richard Mbuguni wakidai amechangia kusababisha umaskini kwa
wakulima.
Mgogoro kati ya mwekezaji na wakulima, ulianza mwaka 2002 na kuendelea mwaka 2008 ambapo
Mei 26, 2013 kiwanda kilifungwa.
Chapisha Maoni