Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limelaani kitendo cha askari wake wa kikosi cha Nyandoto 27 KJ Makoko ambaye inadaiwa alishindwa kutii
maelekezo ya askari polisi wa Usalama
Barabarani wilayani Tarime, Mara na kusabisha mapigano baina ya wanajeshi na polisi.
Katika tukio hilo ambalo lilitokea Oktoba Mosi, mwaka huu jioni katika kituo cha mabasi mjini Tarime, raia mmoja na askari kadhaa wa Jeshi la
Polisi wakiongozwa na Mkuu wa Upelekezi wa Makosa ya Jinai (RCO) Kanda maalum ya Tarime /Rorya na askari wawili wa JWTZ walijeruhiwa kwa risasi.
Mkuu wa Brigedi 202 kundi la vikosi kanda ya Magharibi, Brigedia Jenerali Mathew Mayela Sukambi, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa
Majeshi, alisema kitendo hicho cha aibu
kimefanywa na askari binafsi na siyo JWTZ.
Alisema askari huyo amekiuka kiapo chake, hivyo hastahili kuendelea kuitwa mwanajeshi wa jeshi hilo na kwamba ameagiza sheria na taratibu
zichukuliwe dhidi yake pamoja na wote
walioshiriki katika tukio hilo.
“Kitendo hicho kimefanywa na askari binafsi na siyo jeshi, taratibu za jeshi zinafundisha na kueleza afisa na askari kuwa mtiifu na mwenye nidhamu na kutakiwa kutii mamlaka na kufuata
sheria za nchi kwa mujibu wa katiba,” ilieleza sehemu ya tamko hilo la JWTZ.
Alisema kuwa chanzo cha fujo na vurugu hizo zilisabishwa na askari wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kumkamata askari wa
JWTZ kwa kosa la kuendesha pikipiki bila kuvaa kofia ngumu (Helment) na baada ya majibishano askari huyo aliita wenzake waliokuwa jirani kwa
ajili ya msaada ndipo polisi waliitana kwa wingi na kuanza kutumia nguvu kwa kutumia risasi za moto kuzima vurugu hizo.
Aliwataka maofisa na askari wa jeshi hilo kuzingatia viapo vyao, kutii sheria na taratibu za nchi, mamlaka ya kiraia kwa mujibu wa katiba ya Tanzania huku akiwaonya raia kuacha kushabikia
matukio mabaya pindi yanapotokea.
Chapisha Maoni