MWANZILISHI wa mashindano ya urembo ya Miss Tanzania, Prashant Patel, amefungua maombi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akiomba mshirika wake, Hashim Ludenga, azuiliwe kuendelea kuendesha mashindano hayo
yanayotarajiwa kufikia kilele chake Oktoba 11, mwaka huu.
Patel amewasilisha maombi hayo katika hati ya dharura kupitia wakili wake, Benjamin Mwakagamba, akidai Lundenga ana mpango wa
kuendesha mashindano hayo kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, kinyume cha sheria na bila hata kumtaarifu.
Anaomba mahakama itoe zuio dhidi ya Lundenga, la kuendesha mashindano hayo hadi shauri lake la msingi aliloliwasilisha litakaposikilizwa na
kutolewa uamuzi.
Katika kesi yake ya msingi, Patel anadai pamoja na mambo mengine, utekelezaji wa makubaliano ya Februari 20, 2012 na malipo ya Sh milioni 19 ambayo hayajalipwa kwa mujibu wa mkataba na
faida nyinginezo ambazo zimejitokeza hadi Septemba 23, mwaka huu.
Shauli hilo limepangwa kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Frank Moshi leo, na Lundenga
ametakiwa kuwasilisha utetezi wake ndani ya siku 21, na akishindwa kufanya hivyo, mahakama itaendelea kutoa hukumu dhidi yake.
Katika hati ya kiapo inayounga mkono maombiByake, Patel anadai kuwa yeye pamoja na Lundenga ndio waanzilishi, waongozaji na waendeshaji wa mashindano ya Miss Tanzania na
wamekuwa katika hali hiyo kwa miaka 20 sasa, tangu mashindano hayo yaliyoporuhusiwa tena mwaka 1994.
Kwa kipindi chote hicho, wamekuwa wakisaini makubaliano ya namna ya kuendesha mashindano hayo na mara ya mwisho walisaini makubaliano
Februari 20, 2012.
Hata hivyo, Lundenga alikataa kusaini
makubaliano kwa mwaka 2013 na 2014 na ameshindwa kumlipa fedha zake Sh milioni 19. Patel anadai badala yake Ludenga ameshirikiana na wadhamini wengine kuendesha mashindano
hayo.
Kwa mujibu wa makubaliano, Lundenga pia alipaswa kulipa pauni za Uingereza 30,000 kama malipo ya kibali kwa mwendeshaji wa shindano
hilo duniani, Miss World, deni ambalo limekuwa la muda mrefu, hivyo kuchafua hadhi yake.
Patel anadai kuwa Ludenga alipelekewa taarifa na wakili wake kulimaliza suala hili bila kushirikisha hatua za kisheria, lakini alikaidi na kukataa. Hivyo
Patel anadai kuwa hakuwa na njia nyingine zaidi ya kulipeleka suala hilo mahakamani.
Chapisha Maoni