0
Watu 13 wakiwamo wafanyakazi tisa wa Benki ya Stanbic jijini Dar wanashikiliwa na polisi baada ya majambazi kuiba fedha zaidi ya Sh1 bilioni jana
jioni.

Watu hao wanashikiliwa katika Kituo cha
Oysterbay kwa uchunguzi zaidi wa uporaji huo uliofanywa na majambazi yenye silaha yaliyoingia katika Tawi la benki hiyo la Mayfair Plaza lililopo
Barabara ya Mwai Kibaki na kutokomea na kitita hicho.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, amesema kuwa watu wengine wanne wanaoshiliwa ni askari aliyekuwa lindo na wengine
watatu ambao hakuwa tayari kuwataja.
Wambura ndiye aliyeongoza kikosi cha askari kanzu na wenye sare kufanya uchunguzi wa awali katika jengo la benki hiyo ili kujiridhisha na kilichotokea katika tukio hilo. Alisema kiasi kamili
cha fedha zilizoibwa kitatolewa baadaye baada ya polisi kukamilisha uchunguzi wao.

“Siwezi kusema leo moja kwa moja kiasi kamili cha fedha zilizoibwa kwa sababu kila mmoja tuliyemhoji anatoa kiwango tofauti,” alisema Wambura.
Hata hivyo, chanzo chetu cha habari ambacho hakikutaka kitajwe, kilidai kuwa hadi jana alasiri, maofisa wa benki hiyo waliokuwa wanashiriki
uchunguzi, walibainisha kuwa kiasi cha zaidi ya Sh1.0943 bilioni kilikuwa kimeibwa.

Chanzo hicho kilibainisha kuwa kiwango hicho cha fedha kinajumuisha sarafu mbalimbali zikiwamo fedha za Tanzania, Euro, Pauni na Dola za Marekani.
Habari zilizopatikana baadaye kutoka katika chanzo chetu, zilidai kuwa fedha zilizoibwa ni Euro 260,000 (Sh598 million), Dola za Marekani
175,000 (Sh280milioni), Sh216 milioni za
Tanzania, na pauni 190 za Uingereza
(Sh380,000).


Mwananchi

Chapisha Maoni

 
Top