0
Rais Jakaya Kikwete amewakemea wakuu wa mikoa na wilaya wanaokaa ofisini wakisubiri kuletewa taarifa bila kujua kinachoendelea katika
maeneo yao.

Amesema viongozi wa aina hiyo hawafai kuwapo kwenye nafasi hizo. Aidha, aliwataka kukamilisha agizo lake la kujenga maabara katika halmashauri
zao na kuwa Desemba 9, mwaka huu atakagua shule zote.

Alitoa agizo hilo mjini Dodoma wakati akifungua kikao cha kazi cha usimamizi na uendeshaji wa masuala ya elimu ya msingi na sekondari kwa viongozi hao.

Alisema lazima kila halmashauri ihakikishe imekamilisha ujenzi wa maabara ya Biolojia, Fizikia na Kemia ifikapo Novemba mwaka huu.
Alisema katika hilo hatakuwa na msalie Mtume na ataanza kwa kuwawajibisha wakurugenzi na wengine watafuata.

“Nashukuru Mungu huwa sina tabia ya kusahau, sitasahau nitauliza muda wangu nilioupanga ukifika, kama vile ninavyoyakumbuka majina yenu
ndivyo nitakavyokumbuka kuuliza, sijisifii lakini nina uwezo mkubwa wa kumbukumbu sasa usijidanganye,” alisema Kikwete.

“Mkuu wa mkoa na wewe wa wilaya wewe kazi yako kuingia asubuhi ofisini na kuuliza kama kuna barua yoyote, msisubiri kuletewa taarifa mimi mbona najishughulisha nayajua haya yote
kila wilaya kwanini nyie msijue wakati ndio wawakilishi wa rais? Mnatakiwa kujishughulisha asiyefanya hivyo ni bora asiwepo," alisisitiza.

Alihoji kama suala la ukuu wa wilaya na ukuu wa mikoa ni kusimuliwa tu nini kazi zao. “Maendeleo ya nchi hii yapo kwa mkurugenzi, sasa kama hayakukereketi ni bora ukafanya kazi nyingine
kwanini uwepo na kwanini uendelee…Hawa wengine nawabana tu kwa sababu ni wawakilishi wangu akijibu ninachomuuliza naona hatoshi tu,
mkuu wa wilaya ni masters of voice (bwana wa sauti) wakurugenzi ndio kila kitu kutimiza wajibu wao,” alisema.

Alisema, masomo ya Sayansi lazima yaende na vitendo kwenye mitihani yake, mwanafunzi asipokuwa na maabara hizo katika shule kamwe
hawezi kufaulu mitihani hiyo.
Aliongeza kuwa nchi lazima iwe na wanasayansi na kwamba elimu bila Sayansi haikukamilika.

Aidha alisema maendeleo wanayoyajua wananchi si kusema majukwaani bali ni vitendo. Akizungumzia ujenzi wa madarasa ya kidato cha tano na sita, aliwaagiza viongozi hao kuhakikisha
wanajenga madarasa hayo pamoja na mabweni ili kuwawezesha wanafunzi wanaofaulu kidato cha nne kuendelea na masomo.

Alisema shule hizo hazitakuwa za kata bali zitakuwa za kitaifa kwa lengo la kuwajengea vijana utaifa na uzalendo.
Alisema shule za kidato cha tano na sita
zilizojengwa kwa ajili ya kata zibadilishwe na kuwa za kitaifa ili vijana hao waweze kujua nchi.
Aliwahimiza kuendelea kujenga shule za sekondari kutokana na ongezeko la wanafunzi.

Aidha alisema hakuna mwanafunzi mwenye sifa aliyekosa kwenda chuo kikuu kutokana na vyuo hivyo kuwa vingi nchini na vinadahili wanafunzi
wengi na wakati mwingine kukosa wanafunzi wenye sifa.

“Kwa kiwango hicho tumepita wakenya na waganda ambao awali walikuwa mbali sana kielimu Tanzania ni nchi kubwa inazidi Kenya na Uganda ambao awali walituzidi idadi ya
wanafunzi, msingi, sekondari na vyuo
vikuu,” alisema Kikwete.

Hata hivyo, aliwataka kutazama ubora wa elimu unaotolewa kwa kuhakikisha kunakuwepo na walimu wa kutosha wenye sifa katika kila somo,
kuwepo na vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na vitabu.

Kuhusu vitabu, Kikwete alisema atahakikisha ifikapo 2016 kila mtoto awe na kitabu chake kila somo tofauti na sasa ambapo kitabu kimoja kinatumiwa na wanafunzi watatu.
Suala la upungufu wa madawati, Rais alisema ni aibu wanafunzi kuendelea kukaa chini na jambo
hilo halikubaliki.

Chapisha Maoni

 
Top