KESI ya kutumia lugha ya matusi na kutotii amri ya askari wa usalama barabarani, inayowakabili watangazaji wawili, Ephrahim Kibonde wa Kituo
cha Habari cha Clouds Media Group na Gadner Habash wa Times Fm, imeahirishwa hadi Novemba 5 na 12 mwaka huu itakapoanza
kusikilizwa.
Watangazaji hao waliiomba mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni kuahirisha kesi hiyo kutokana na wakili wao kupata dharura na waliomba tarehe
nyingine ya kusikiliza shauri hilo.
Hakimu Anicetha Wambura alikubaliana na ombi hilo licha ya kuwepo kwa shahidi na kusema kwamba shauri hilo litaanza kusikilizwa Novemba
5 na 12 mwaka huu.
Awali, Wakili wa Serikali Ramadhan Mkimbu aliwasomea mashitaka yao na kudai kwamba Agosti 9 mwaka huu, eneo la Oysterbay jirani na
kituo cha Polisi washitakiwa walitumia lugha ya matusi na kusababisha uvunjifu wa amani.
Pia Kibonde alidaiwa kukataa kutii amri ya halali ya askari E44190 Koplo Sweetbert aliyemtaka arudishe gari lake lenye namba T 459 CPL aina ya
Toyota Brevis kwenye eneo alilosababisha ajali, badala yake alikimbia na kukamatwa.
Chapisha Maoni