0
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika yaUmma (PAC), imetoa siku mbili kwa uongozi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)
kuwasilisha mikataba 26 ya gesi kwa Katibu wa Bunge.

Uamuzi wa kamati hiyo umetokana na
menejimenti ya TPDC kushindwa kuwasilisha mkataba hata mmoja kati ya mikataba 26 iliyoombwa na kamati hiyo katika kipindi cha mwaka mmoja sasa.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa kupitia hesabu za shirika hilo, Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, alisema viongozi hao pia wanapaswa
kuwasilisha mapitio ya mikataba hiyo sambamba na taarifa ya bomba la gesi.

Alisema katika tafsiri ya utendaji kazi wa kamati, viongozi wanapaswa kuwasilisha mikataba hiyo pale inapohitajika kwenye kamati ili wajumbe
waipitie na kuijadili.
Zitto alisema kamati hiyo imepewa nguvu ya kisheria ya kuwajibisha shirika lolote ambalo halitakuwa tayari kutoa ushirikiano pamoja na kuwasilisha taarifa zake pindi zinapohitajika.
“Kwa kosa mlilolifanya la kugoma kuja na taarifa za mikataba yenu mbele ya kamati hii, mnataka tuwafanyeje? Je, tuwawajibishe kwa kosa hili?”
alihoji Zitto.
Akijibu hoja hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya TPDC, Michael Mande, alisema uamuzi wa kutowasilisha mikataba hiyo unatokana na kutoruhusiwa
kisheria kuwasilisha mikataba ya aina hiyo mbele ya kamati hiyo.

Alisema badala yake sheria inawataka kuipeleka kwa Waziri wa Nishati na Madini.B“Tumeshindwa kuleta taarifa zetu mbele ya kamati kwa sababu sheria haituruhusu kutoa taarifa ya mikataba mbele ya kamati, tunachotakiwa kufanya
ni kuiwasilisha katika ofisi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Mande.

Hoja hiyo ilipingwa na Katibu wa Kamati, Erick Maseke, ambaye alisema sheria inatoa ruhusa kwa kamati kupewa mikataba yote isipokuwa iliyo
na mlengo wa kuhatarisha usalama wa nchi.
Baada ya ufafanuzi huo, Mande alisema kutokana na kujitokeza kwa migongano ya kisheria, aliiomba kamati isitoe adhabu kwa shirika hilo kwa kosa walilofanya.
“Hapana… tusifike huko, kama mikataba
tungekuwa nayo hapa tungetoa ila kwa hapa tuna ‘copy’ (vivuli vya mikataba) na ‘original’ zake zipo kwa Waziri wa Nishati na Madini,” alisema
Mande.
Baada ya kusema hivyo, Zitto aliitaka Bodi ya TPDC kesho kuwasilisha mikataba saba iliyofanyiwa ukaguzi na Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) ikiwamo mingine 19
ambayo haijakaguliwa hesabu zake.
“Mikataba hii ifike kwenye ofisi ya Katibu wa Bunge siku ya Jumatano saa za kazi, ikiwamo mikataba yote iliyofanyiwa michanganuo,” alisema
Zitto.

Chapisha Maoni

 
Top