0
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini,IGP Ernest Mangu akizungumza na Mtendaji wa Kijiji cha Chekanao, Kata ya Kiperesa , Wilayani Kiteto Bw.Omar Ndee (kulia) wakati alipofanya ziara wilayani humo kufuatia kuwepo kwa migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji iliyosababisha kutokea mapigano yaliyosababisha kutokea kwa vifo.


Katikati ni Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Manyara, Deusdedit Nsimike
pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji hicho
Bw.Japhet Chafu (Picha na Frank Geofray- Jeshi la Polisi)
Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi, Kiteto.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Ernest Mangu ameahidi kuongeza idadi ya Askari katika kijiji cha Chekanao, kata ya Kiperesa
wilayani Kiteto Mkoani Manyara kufuatia
wananchi katika kijiji hicho kujitolea
nyumba kwa ajili ya kuishi Askari kwa
lengo la kuimarisha usalama katika
maeneo yao kufuatia kuwepo kwa migogoro ya ardhi inayosababisha kutokea kwa mauaji.

IGP Mangu aliyasema hayo jana wakati
alipokuwa katika ziara Wilayani Kiteto ya
kujionea uharibifu uliojitokeza pamoja na kutafuta ufumbuzi wa migogoro hiyo
iliyopelekea kutokea kwa vifo vya wakulima na wafugaji hivi karibuni katika wilaya hiyo ambapo watu kadhaa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kutokana na vurugu hizo.

Alisema kufuatia kuwepo kwa umbali mrefu wa kituo cha Polisi na kijiji hicho
atahakikisha askari wa kudumu
wanakuwepo ili kushirikiana na wananchi katika kuwabaini wahalifu wanaofanya vurugu na kuendeleza migogoro hiyo ambapo wananchi nao waliahidi kujenga kituo cha Polisi.

Kwa upande wake Mtendaji wa Kijiji cha
Chekanao Bw.Omar Ndee alisema
wamekuwa wakipata shida kutokana na
umbali mrefu wa kituo cha Polisi jambo
ambalo limekuwa likifanya kuongezeka kwa
vitendo vya uhalifu vinavyochangiwa na
migogoro ya ardhi katika wilaya ya Kiteto.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji hicho Japhet
Chafu alilishukuru Jeshi la Polisi kwa
kuimarisha usalama kijijini hapo tangu
kutokea kwa mauji ya wakulima na
wafungaji ambapo alibainisha kuwa bila
kuwepo wao hali ingekuwa mbaya zaidi
kutokana na kutokuwepo na muafaka
baina ya wakulima na wafugaji.
“IGP hawa askari wako wasingekuwepo
hapa usingekuta mtu lakini tunawashukuru sana hawa askari kwa kuwa hivi sasa hali
ya usalama imerejea na hata shambani
tumeanza kwenda” Alisema Bw.Chafu.
IGP Ernest Mangu alitumia ziara hiyo
kuzungumza na Mkuu wa Wilaya ya Kiteto,
kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya,
Wakaguzi wa Tarafa pamoja na Askari
Kata ili kutafuta ufumbuzi wa migogoro
hiyo na kuimarisha hali ya ulinzi na
usalama.

Chapisha Maoni

 
Top