SERIKALI Kuu kwa kushirikiana na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya Handeni na Mkoa mzima wa Tanga, wameombwa kuingilia kati mgogoro mzito wa ardhi katika kijiji cha Komsala, wilayani Handeni, ili kuepusha hatari inayoweza kutokea, ikiwamo vita ya wenyewe kwa wenyewe.
Hayo yamesemwa juzi na wananchi wa
kijiji hicho katika mkutano ulioandaliwa na taasisi ya Handeni Kwetu Foundation
inayofanya ziara katika maeneo
mbalimbali, hususan ya wilaya ya Handeni, mkoani Tanga, baada ya kuzinduliwa Mei 8
mwaka huu.
Wakizungumza kwa uchungu mkubwa,
wananchi hao walisema kuwa hali ni
mbaya, maana kijiji chao kimeendelea
kutekwa na kubaki eneo dogo lililoanza
kuibua chuki za wazi kwa wananchi.
Mzee aliyejitambulisha kwa jina la Alhaj
Ally Yasin Ling’ande, alisema kiuhalisia
hakuna kijiji cha Komsala, kwakuwa
hawana eneo la ardhi, hasa baada ya
wilaya Korogwe kuingia kwenye eneo lao
kwa kufikia hata kujenga mnada wa
ng’ombe.
“Ukiaangalia usawa palipojengwa mnada, utaamini kuwa hata kwenye shule ya Msingi Komsala pia patakuwa ni eneo la Korogwe, ingawa si sahihi kulinganaa na ramani ya mwaka 1978, jambo linaloonyesha kuwa
huu ni mzozo utakaoweza kumwaga damu,” alisema.
Naye William Seif alisema mbali na mipaka hiyo kuwa tata, pia kumekuwa na idadi kubwa ya wageni kumiliki heka zaidi ya 130 na bado wanaingia kwa wenye heka tatu wakiamini kuwa uwezo wao kifedha unawafanya wamudu kesi zinazoendeshwa kwenye mabaraza ya Kata na wao kupata haki.
“Masikini akionewa anakimbilia kwenye
Bazara la Kata, lakini huko kumekuwa na
danadana nyingi, ukizingatia kuwa siku
zote mkono mtupu haulambwi, ndio maana
tunaoimba serikali ya wilaya ya Handeni,
mkoa na wadau wengine wa ardhi kuja
kujionea bomu hili linalosubiriwa kuripuka hapa kwetu,” alisema.
Mwananchi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Bashiri Wabu, alisema kuwa ardhi katika kijiji chao imeuzwa kiholela kwa watu wenye nazo bila kufuata sheria za ardhi, ikiwamo ya kuandaa mkutano wa wananchi wote.
“Kuna watu hawana maeneo kabisa ya
kulima, wakati watu wachache wanamiliki maeneo makubwa ambayo hata kuyalima yote hawana uwezo huo, jambo linalokera na kuudhi mno kila tunapoliangalia suala
hili katika kijiji chetu,” alisema Wabu,
akiungwa mkono pia na Hemed Ngona,
Kombo Twaha, wakisisitiza kuwa sheria za ardhi na utawala bora hazifuatwi katika kijiji chao.
Katika mkutano huo ulioanza saa 9 alasiri na kumalizika saa 12 jioni, ulihudhuriwa na watu wengi, huku idadi kubwa ikiegemea katika kero ya ardhi na mipaka.
Aidha Mwenyekiti wa kijiji cha Komsala
anayemaliza muda wake, Mwanaidi Said,
alisema kero kubwa katika kijiji hicho ni
mipaka iliyoshindwa kutatuliwa na
viongozi wa juu, licha ya kupeleka
malalamiko yao mara kadhaa.
“Kijiji cha Komsala sasa ni kama kitongoji tu, maana kimechotwa katika pembe zote na ndio maana hata wenzetu wa Korogwe wamekuja kujenga mnada wa ng’ombe kwa
madai kuwa ni kwao, jambo ambalo hata
mwenyekiti atakayefuata litamuumiza
kichwa,” alisema na kuwafanya wananchi wapatwe na hofu.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo aliyetumia muda huo kuaga wananchi wake, sekeseke la mipaka limeshindwa kutatuliwa, huku
akiwataka viongozi kulipa kipaumbele
kabla ya matatizo hayajakikumba kijiji
chao pale wananchi hao watakapotafuta
haki yao.
Naye Msemaji Mkuu wa taasisi hiyo, Kambi Mbwana, aliwashukuru viongozi wa serikali ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kwa
kuwapa ushirikiano, ikiwamo kuruhusu
kutembelea katika vijiji mbalimbali kutoa
elimu ya uraia na kuhamasisha utawala
bora.
“Naomba niwatoe hofu Watanzania wote
kuwa mikutano hii ya hadhara hairatibiwi na chama chochote cha siasa, hivyo tunaomba tushirikiane kwa ajili ya kufanikisha maendeleo, hasa kama wananchi watahudhuria mikutano
wanapoitwa na viongozi wao,” alisema.
Ziara ya Handeni Kwetu Foundation
ilianzia Kata ya Misima, ambapo wananchi wengi wameiunga mkono taasisi hiyo yenye lengo la kuwakomboa wananchi kwa kutoa elimu na kuhamasisha maendeleo ya jamii.
Chapisha Maoni