Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia Baraza lake la vijana, kimetangaza kuzindua Bavicha Operesheni itakayohusisha matumizi ya chopa kuzunguka katika mikoa ya
kanda za Kati na Magharibi kueneza ujumbe wa kuikataa Katiba Inayopendekezwa sambamba na
kujipanga kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Operesheni hiyo itakayojumuisha mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi kwa Kanda ya Magharibi na Kati, itakuwa na mikoa ya Singida, Dodoma na Morogoro na itafanywa na viongozi wa Bavicha Taifa ikiwa na lengo la kurejesha haki
na usawa kupitia Serikali za Mitaa.
Mwenyekiti wa Bavicha, Paschal Katambi alisema jana kuwa mpango huo ni mfululizo wa mkakati wa chama hicho kuelekea Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa, kuimarisha chama pamoja na Katiba na mkakati ulioanzishwa na Bawacha katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Alisema kutakuwa na timu za watu 30
watakaokuwa wanazunguka katika majimbo yote ya mikoa hiyo ambao watatumia usafiri wa magari.
“Kila timu itazunguka katika kanda husika isipokuwa mwenyekiti ambaye atakuwa kwenye chopa. Yeye atalazimika kuzunguka mikoa yote,
tunatarajia kuwafikia wananchi wengi na kuwapa ujumbe wa kuipigia kura ya hapana Katiba Inayopendekezwa,” alisema.
Mwenyekiti huyo alisema chama tawala licha ya kuichakachua Katiba hiyo, bado hakijatoa nakala za kutosha na kuzisambaza kwa wananchi wote
ili waisome kabla hawajafanya uamuzi sahihi muda utakapofika.
Naye katibu mkuu wa Bavicha, Julius Mwita alisema pamoja na mikutano ya hadhara, wanatarajia kufanya semina kwa viongozi walioko mikoani kuanzia ngazi ya mtaa hadi jimbo kwa
lengo la kuwajengea uwezo.
“Tumedhamiria kushinda kwa zaidi ya asilimia 50 katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hivyo maandalizi lazima yaanze mapema,” alisema
Mwita.
Aliwataka viongozi wote wa Chadema katika mikoa hiyo, kuhakikisha wanajipanga vyema kupambana na CCM katika maeneo yote ambayo
inayatawala.
“Huu siyo mwaka wa kulala, lazima tufanye kazi kwa kuhakikisha umma unapata elimu ya kutosha ili wafanye uamuzi sahihi,” alisema.
Chapisha Maoni