Katibu wa Hamasa na Chipukizi wa jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM, Paul Makonda amekanusha taarifa ya kwamba amehusika kumpiga Waziri Mkuu wa zamani Jaji Joseph
warioba jana.
Amesema hawezi kumfanyia kitendo kama kile Jaji warioba kwani anamuheshimu kama mzazi wake.
Katika vurugu hizo, Makonda anatuhumiwa kumpiga aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba.
Akizungumza katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Makonda amesema kimsingi hahusiki na vurugu hizo wala kumpiga mzee Warioba kama ambavyo imekuwa
ikidaiwa.
Makonda amewaambia waandishi wa habari kuwa tofauti na uzushi huo, yeye alishiriki kwa kiasi kikubwa kuepusha mzee Warioba asipigwe na vijana waliokuwa wanashiriki vurugu hizo na
kwamba bado ana uhusiano mzuri na mwanasiasa huyo mkongwe nchini.
"Jaji Warioba ni mzee wangu na tumekuwa tukishirikiana katika mambo mengi na ya msingi yanayohusu mustakbali wa nchi..haitakuwa jambo
la kawaida kwa mimi kumdhuru mzee Warioba na kwamba katika kuthibitisha ukweli huo, tangu baada ya tukio hilo nimekuwa nikiwasiliana naye
na tumekuwa tukipeana pole kwa yaliyotokea jana." amesema Makonda.
Ameongeza kuwa wanaozusha uvumi huo ni watu wenye nia ovu juu yake na ambao wanadhani kwa kufanya hivyo watamzima kisiasa, ambapo yeye
mwenyewe amesema hajui walioanzisha vurugu hizo walikuwa na nia gani kwani hawaoneshi kuwa na msukumo wa chama chochote cha siasa.
Mwanasiasa huyo kijana amewataka wale wote wenye hisia potofu juu ya nani hasa mhusika wa vurugu hizo kwenda kuonana na uongozi wa ukumbi wa Ubungo Plaza ili wapatiwe picha za
kiusalama za CCTV ambazo zitaonesha chanzo na nani hasa amehusika na vurugu hizo.
Aidha, ameongeza kuwa wakati vurugu hizo zinaanza, muda mwingi aliutumia kumuokoa mmoja wa washiriki ambaye ni mlemavu wa macho pamoja na Jaji Warioba, lakini cha kusikitisha ni kwamba watu wenye nia mbaya
wanatumia nafasi hiyo kutaka kumchafua kwa faida za malengo yao ya kisiasa.
Baraza la Wazee la Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania limelaani vikali kuvamiwa hapo jana kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba nchini Jaji Mstaafu Joseph Warioba wakati akiwa katika mdahalo wa Katiba inayopendekezwa
uliofanyika Jijini Dar es Salaam.
Wakizungumza leo Jijini Dar es Salaam,
Mwenyekiti wa Baraza hilo Abdallah Tambagwaza na Katibu Mstaafu wa Chama cha Mapinduzi mkoa
wa Dar es Salaam Mohamedi Ligola wamesema vijana wana wajibu wa kuheshimu mawazo ya wazee na hawapaswi kuwadharau kwani kufanya
hivyo ni kwenda kinyume na maadili ya nchi.
Wazee hao wamesema hata katika Bunge Maalum la Katiba kulikuwa na baadhi ya wajumbe walikuwa wakipingana na mchakato wa bunge
lilivyokuwa linaendeshwa lakini kulikuwa na njia bora zilizotumika katika kuleta maridhiano na si vurugu kama ilivyotokea hapo jana.
Chapisha Maoni