0
WAKATI makundi kadhaa yakianza kufanya mikutano na kuendesha midahalo kuhusiana na Katiba Inayopendekezwa, Rais Jakaya Kikwete
amesema muda wa kufanya kampeni na
kuuelimisha umma juu ya katiba hiyo haujafika na amewataka wananchi kuwa na subira ili kuepusha vurugu.

Akilihutubia taifa kupitia mkutano wake na Wazee wa mkoa wa Dodoma jana mjini Dodoma, Rais Kikwete alisema sheria ya kura ya maoni ya
Katiba mpya inaelekeza muda wa wadau
kuuelimisha umma na muda wa kufanya kampeni kabla ya kupigwa kwa kura hiyo.

Alisema kwa mujibu wa sheria hiyo, zimetengwa siku 60, kabla ya kufanyika kwa kura ya maoni kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuandaa utaratibu
wa wadau kuelimisha umma kuhusu Katiba Inayopendekezwa.

Pia alisema kampeni za kukubali au kukataa katiba hizo zitafanyika siku 30 kabla ya siku ya kura ya maoni.

Ataka subira, asifu kazi ya Warioba
“Naomba tuwe na subira, tuzingatie sheria muda wa wadau kuelimisha umma bado haujafika, wana nafasi ya kufanya hivyo na watapewa, lakini tofauti na hivyo ni kuleta vurugu ambazo ndio chanzo cha migogoro,” alisema Rais Kikwete.

Akizungumzia Katiba Inayopendekezwa, Rais Kikwete alisema imejitosheleza kila nyanja na kwamba kazi ya kukusanya maoni iliyofanywa na Tume ya Jaji Joseph Warioba ilikuwa nzuri na
ilitumika kama mwongozo kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, kupata Katiba Inayopendekezwa.

“Niwashukuru wote waliofanikisha mchakato wa kupatikana kwa Katiba Inayopendekezwa, wote wamefanya kazi nzuri na sasa uzuri au ubaya wa
katiba hiyo sio wa kuambiwa na mtu, waacheni wananchi waisome waione na siku ya kura watachagua,” alisisitiza Rais Kikwete.

Alisema wananchi wawe na subira kwani wameagiza nakala nyingi zichapwe za Katiba Inayopendekezwa ili wananchi wengi waipate ,
waisome na kuielewa kisha wapige kura ya kuamua.

“Wananchi msikubali kuhadaiwa, someni wenyewe Katiba inayopendekezwa, mjue kilichopo na sio kudanganywa na watu maana uhondo wa ngoma
lazima uingie ucheze,” alisema Rais Kikwete.

Alifafanua kuwa mara baada ya kukabidhiwa Katiba Inayopendekezwa mjini Dodoma na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba Samuel Sitta, alisema kazi yake kama Rais ni kutangaza
siku ya kuchapishwa kwenye gazeti la Serikali.

Kura za maoni Alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iliomba muda zaidi wa kufanya matayarisho ya jinsi ya
kuitisha kura hiyo kwa kuwa mfumo mpya utatumika kuandikisha wananchi wote upya wenye lengo la kuziba mianya ya wizi au mtu mmoja kuandikishwa mara mbili.

“Kura ya maoni itaitishwa Aprili 30, mwakani na siku 60, kabla ya kura hiyo kumeandaliwa utaratibu kwa mujibu wa sheria kwa wadau kuelimisha umma,” alisema Rais Kikwete na kuongeza ikiwa katiba hiyo itakataliwa, basi kura
ya maoni itarudiwa mwezi Juni.
Uchaguzi Serikali za Mitaa Kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Rais
alisema utafanyika Desemba 14, mwaka huu ambapo wananchi kuanzia ngazi ya mitaa, vitongoji na vijiji watachagua viongozi wao na kwamba kazi ya uandikishaji wapigakura itaanza
Novemba 27 hadi 30.

Aidha alivikumbusha vyama vya siasa nchini ambavyo vitasimamisha wagombea wake kwenye nafasi hizo kuwasilisha kwa wakati majina ya
wagombea wao kwa msimamizi wa kituo cha kupiga kura, ili kuepuka usumbufu.

Hata hivyo alisema kazi ya kunadi wagombea wa vyama vya siasa itaanza Novemba 30 na kumalizika Desemba 13 ikiwa ni siku moja kabla
ya uchaguzi wenyewe.

Alisisitiza kuwa, ni vyema wananchi wakawa makini na aina ya viongozi wanaowachagua na kwamba wakichagua viongozi wazuri watakuwa
wamejenga msingi bora.

“Chagueni wanaopenda utulivu na sio vurugu, kwa maana mkishamchagua mtu ovyo mtajuta… halafu ndio kwanza yuko madarakani itabidi mvumilie kwa miaka yake yote ya uongozi, ila
mkichagua kiongozi mzuri mtaendeleza utulivu na maendeleo,” alionya Rais Kikwete.

Kuhusu ebola Akizungumzia ugonjwa wa ebola, Rais Kikwete alisema Watanzania wanapaswa kuchukua
tahadhari dhidi ya ugonjwa huo, ingawa haijaingia nchini.
Alisema kasi ya kuenea kwake ni kubwa na kwamba unapoingia, unaleta madhara makubwa hivyo hatuna budi kuchukua hatua za kujikinga na
kuhakikisha mipaka yote ya nchi na viwanja vya ndege vinakuwa na tahadhari hiyo.

Alishauri wananchi kutoa taarifa endapo wataona mtu au kuwa na dalili za ugonjwa huo, ambazo baadhi yake ni homa kali, kutokwa na damu
kwenye matundu mbalimbali ya mwili na kutapika.
Dk Shein aonya wachochezi
Wakati Rais Kikwete akiusihi umma kuachana na michakato ya kampeni za kuelimisha umma juu ya Katiba Inayopendekezwa hadi hapo muda
mwafaka utakapofika, Rais wa Zanzibar, Dk Ali
Mohamed Shein amewataka viongozi wa vyama vya siasa kuacha kutumia vibaya mchakato wa Katiba Inayopendekezwa kwa lengo ya kuwagawa
wananchi na kutishia amani na utulivu uliopo nchini.

Lakini pia ameelezea kukerwa na kuchoshwa na
matusi yanayojitokeza katika kipindi hiki kutoka
kwa baadhi ya viongozi, huku akisema
atawachukulia hatua za kisheria na za kinidhamu bila kujali wana nyadhifa gani.

Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wananchi na viongozi wa CCM katika maadhimisho ya miaka minne ya kuwepo madarakani tangu aliposhinda Urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2010.

“Nitawachukulia hatua za kisheria na kinidhamu viongozi wanaotumia vibaya mchakato wa kupata Katiba mpya kwa kutoa kauli za chuki na kutukanana katika majukwaa… nitatumia Katiba na
Sheria na sio ubabe kwa sababu sio kawaida yangu kufanya hivyo,” alisema.

Alisema kumeanza kujitokeza viashiria vya kuanza kuvuruga amani na utulivu iliyopo sasa kwa kisingizio cha mchakato wa rasimu ya Katiba
Inayopendekezwa hivi sasa.
Alisema Katiba Inayopendekezwa ni mkombozi kwa wananchi wa Zanzibar kwa sababu imejibu hoja za malalamiko na kero za Muungano ambazo awali zilikuwa zikilalamikiwa na wananchi
ikiwemo wanasiasa.

Akifafanua, alisema kwa muda mrefu wananchi wa Zanzibar walikuwa na malalamiko mengi katika Muungano ambayo kwa bahati nzuri katika Katiba
Inayopendekezwa yamepatiwa jawabu sahihi. 
Kwa mfano alisema si kweli kwamba Muunganobuliopo sasa umeimeza Zanzibar na haitambuliwi katika jumuiya za kimataifa ikiwemo Umoja wa Mataifa.

Chapisha Maoni

 
Top