0
Siku moja baada ya Kamati ya PAC kuweka hadharani uchunguzi wa Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuhusu Akaunti ya Tegeta Escrow, watu wa kada
mbalimbali wamependekeza hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika.

Zanzibar
Viongozi wa upinzani Zanzibar wamesema wote waliotuhumiwa kuhusika na vitendo vya ufisadi
kupitia Akaunti ya Tegeta Escrow wafukuzwe pamoja na kufunguliwa mashtaka badala ya kuendelea kusubiri msimamo wa Rais katika
jambo hilo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Viongozi wa Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na Tadea walisema
kiwango cha fedha kilichoibiwa ni kikubwa na haikubaliki kwa nchi inayoheshimu misingi ya
utawala bora.

Makamu Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi Zanzibar, Ambar Khamis Haji alisema viongozi walioguswa na ripoti ya uchunguzi lazima wawe watu
waugwana waondoke katika nyadhifa zao wenyewe wasubiri sheria ichukuliwe mkondo wake.

Alisema pamoja na viongozi wa dini na majaji walioguswa katika kashfa ni wakati mwafaka na wao kujiuzulu kutokana na kitendo chao cha
kudhalilisha mamlaka wanazoziongoza wakati wao wanatakiwa kuwa mfano bora katika jamii.

“Pamoja na kwamba fedha za sadaka huwa hazichagui fedha halali au chafu hatuamini kama zilikuwa za kanisa kutokana na kutumika kwa
akaunti ya mtu binafsi,” alisema Ambar.

Mkurugenzi wa Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salim Bimani Abdallah alisema Serikali nzima inapaswa kujiuzulu kutokana na ukubwa wa kashfa.

“Rais wetu ni mtendaji siyo kama mfalme, haiwezekani kufanyike wizi mkubwa kama huo bila ya kufahamu na kuchukua hatua mapema, Serikali nzima ivunjwe kuitishwe uchaguzi,”
alisema Bimani.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Said Issa Mohamed alisema wakati umefika kwa wananchi kujifundisha na kuwa makini wanapofanya uamuzi
ya viongozi kwa sababu CCM imeshindwa kupambana na vitendo vya ufisadi katika Serikali yake.

Alisema inasikitisha, wakati Sh306 bilioni zikipotea, wananchi wanakabiliwa na matatizo makubwa ya kuanguka huduma za jamii.

“Dawa hakuna wanafunzi wanasoma chini ya sakafu huku wengine wakikosa mikopo ya elimu ya juu, wazazi wakilazwa chini kutokana na uhaba
wa vitanda hospitali za Serikali.

“Katika misingi ya utawala bora wanahitajika kujiuzulu kabla ya kufukuzwa na Rais ili sheria
ichukue mkondo wake na mali zao zitaifishwe,” alisema Katibu Mkuu wa Tadea, Juma Ali Khatibu.

Arusha
Wakazi wa Mkoa wa Arusha, wameshinikiza kuwajibika viongozi wa Serikali ambao wamehusika katika kashfa ya kuchotwa fedha
katika Akaunti ya Tegeta Escrow kwani ushahidi upo wazi kuwa kuna mazingira ya kifisadi.

Mmoja wa wakazi hao, Calist Lazaro alisema kitendo tu cha kusambazwa fedha kwa viongozi wa Serikali, wanasiasa na vyombo vya dola kama
Mahakama kunathibitisha mchezo mchafu.

“Nimemsikiliza Waziri Muhongo hakuna alichojibu ametoa historia, sisi tunataka Rais Jakaya Kikwete arudi kuwang’oa viongozi wote na kesi zao zianze,” alisema mkazi huyo wa Boma Ng’ombe..

Mkurugenzi wa Golden Rose Hotel, Walter Maeda alisema anaunga mkono taarifa ya PAC ya kuanzishwa kitengo cha kesi kubwa za rushwa hapa nchini ili kudhibiti wizi kama wa escrow.

“Ninaona wamejitahidi kufanya kazi na wana ushahidi wao nadhani hili litawanufaisha Watanzania milioni 48,” alisema.
Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji wadogo wa madini Mkoa wa Arusha, Sadiki Mnenei alisema taarifa ya PAC imejaa ukweli na ana imani Serikali
itatekeleza maazimio yote.

Mkazi mwingine, Nicholaus Malile alisema PAC, CAG na Takukuru wamefanya kazi kubwa ambayo
inapaswa kupongezwa kwa kufichua wizi na mabilioni ya fedha za umma.

Kigoma
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, walisema licha ya mapendekezo yaliyotolewa, bado kuna haja
kwa watuhumiwa wote waliohusika kuchota fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow kufilisiwa mali zao na kufungwa jela endapo watapatikana na hatia ya
wizi au kufumbia macho wizi huo.

Wakazi wengine, Ibrahim Saidi, Azizi Ally, Boniface Justine, Abdilahi Kalamtana, Kitwazi Omari, Madugu Aloyce, Saidi Hussein, Bakari Saidi na Casian Bernard kwa nyakati tofauti walisema ili
kurudisha imani ya wananchi iliyopotea hakuna budi watuhumiwa hao kuchukuliwa hatua kali za
kisheria.

“Haiwezekani wanyonge wanafungwa jela kwa makosa ya kuiba kuku lakini hawa vigogo eti waachwe licha ya kupora mabilioni ya shilingi.

Hospitali hazina dawa na leo hii tunachangishwa kwa nguvu michango ya ujenzi wa maabara za
sekondari, hili haliwezekani hata kidogo.” alisema Kalamtana.

Mwanza
Akizungumzia suala hilo, Betty Mwakitalu alielezea kusikitishwa na Benki ya Mkombozi inayomilikiwa
na Kanisa Katoliki kutajwa katika sakata hili la aibu.

Kwa upande wake, Bernard Madata alisema: “Watu waliwaamini wakawaweka madarakani hivyo
haistahili kufukuzwa kazi tu, bali wafilisiwe pamoja na kufikishwa kwenye vyombo vya kisheria,” alisema.

Manyara
Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Manyara,
wameipongeza PAC kwa kutoa mapendekezo mazuri bungeni juzi.

Mkazi wa Nyunguu mjini Babati, John Tluway aliwapongeza Mwenyekiti wa PAC, Zitto na Makamu Mwenyekiti wake, Deo Filikunjombe kwa
kusoma taarifa makini.

Chapisha Maoni

 
Top