0
Utangulizi

Taarifa hii inatolewa kwa umma kutokana na ripoti mbalimbali zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari mitandao ya kijamii na taarifa iliyotolewa kwenye mjadala katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

1. Ufunguzi wa akaunti ya VIP engineering and Marketing (VIP)
Kampuni ya VIP engineering and Marketing ni kampuni ambayo imesajiliwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania. 

Kampuni hii ilifungua akaunti katika benki ya biashara ya Mkombozi na hivyo kuwa moja kati ya wateja wa benki. Benki ilijiridhisha na
ilizingatia taratibu zote za ufunguzi wa
akaunti husika kwa kuzingatia sheria za
nchi na kanuni zinazozitaka benki kupata nyaraka muhimu kutoka kwa mteja wakati wa ufunguzi wa akaunti hiyo.

Nyaraka hizo ni pamoja na kuwepo kwa
cheti cha usajili wa kampuni, kanuni za
kampuni, idhinisho la kampuni kumruhusu
moja kati ya wanahisa wake kuendesha
akaunti pamoja na picha na hati ya
kusafiria ya mhusika wa kuendesha akaunti hiyo.

2.0 Mauzo ya hisa za VIP
Kampuni ya VIP ilileta mkataba kwenye
benki ya Mkombozi wa mauziano ya hisa za asilimia 30 baina ya VIP na kampuni ya Pan Africa Power Solutions (PAP) ambazo inamiliki katika kampuni ya IPTL. Mkataba huo ulisainiwa tarehe 19 Ogasti, 2013. Bei ya asilimia 30 ya hisa hizo ilikuwa ni dola za Marekani milioni 75. 

Katika kifungu namba 2.4 cha mkataba wao kinaelekeza fedha za mauzo ya hisa zilipwe kwenye akaunti ya VIP iliyopo benki ya Mkombozi.

Mkataba huo wa mauziano ya hisa baina
ya kampuni hizi mbili ulitambuliwa na
hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania
iliyotolewa na Jaji J.H.K Utamwa tarehe 5 Septemba, 2013.

3. Mchakato wa kulipa kodi ya serikali
Benki ilitambua kwamba katika mauziano hayo ya hisa ni lazima kodi ya Serikali ilipwe na hivyo iliizishauri pande zote mbili kupeleka mkataba husika katika ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kufanyiwa makadirio ya kodi husika.

Tarehe 20 Januari, 2014 TRA iliiandikia
barua kampuni ya VIP na nakala ya barua hiyo kuletwa kwenye benki ya Mkombozi.
Katika barua hiyo TRA iliitaarifu kampuni
ya VIP kuwa makadirio ya kodi yatokanayo na mauzo ya hisa ni shilingi
38,186,584,322.00 ikiwa ni kodi ya mauzo ya hisa ya asilimia 30 za mauzo ya hisa kutoka VIP kwenda kwa PAP.(Capital gains and stamp duty).

TRA pia iliiagiza benki ya Mkombozi
kuhakikisha kuwa inalipa kodi hiyo kwa
niaba ya VIP mara tu fedha zitakapoingia kwenye akaunti yake.

Malipo ya kodi ya shilingi 38,186,584,322.00
yalilipwa TRA kwenye akaunti 11120100
iliyopo katika Benki Kuu ya Tanzania na
TRA ilikiri kupokea kodi hiyo kwa barua
yake yenye kumbukumbu namba
3-4/100/100/223/4 ya tarehe 24 Januari, 2014.

4. Ufafanuzi wa mambo mbalimbali
4.1 Benki ya mkombozi kuhusika katika
kusafisha fedha chafu
Fedha zote zilizoingizwa kwenye akaunti ya VIP iliyopo kwenye benki ya Mkombozi zilitokana na mauziano ya hisa kati ya VIP na PAP kwa mkataba uliotambuliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania. Chanzo cha
malipo hayo ni kuhamisha fedha kutoka
kwenye akaunti ya PAP iliyopo katika benki ya Stanbic na kuingizwa kwenye akaunti ya
VIP iliyopo katika benki ya Mkombozi.
Fedha hizo zilihamishwa katika mafungu
mawili. Fungu la kwanza ilikuwa ni shilingi
73,573,500,000.00 zilihamishwa kwa njia ya TISS kwa kumbukumbu namba 000000050720
ya tarehe 23 Januari, 2014 na fungu la pili ni dola za Kimarekani 22,000,000.00
zilihamishwa kwa TISS kwa kumbukumbu namba000000050812 ya tarehe 23 Januari,
2014. Malipo mengine ya asilimia kumi ya mauzo ya hisa yalilipwa kwenye akaunti ya Mkombozi iliyopo Benki Kuu ya Tanzania.

Kutokana na mchakato huo benki ya
Mkombozi ilijiridhisha kuwa fedha hizo ni
malipo halali na siyo fedha chafu.
Benki ya Mkombozi haijihusishi na
utakasishaji wa fedha chafu na haramu
katika uchumi wa Tanzania.
4.2 Malipo yatokanayo na akaunti ya VIP
Malipo toka kwenye akaunti ya mteja
hufanywa kutokana na maelekezo ya mteja.

Benki ikishajiridhisha kuwa fedha ya mteja ni halali na ipo kwa mujibu wa sheria na hamna zuio lolote toka katika mahakama hapa nchini hutekeleza malipo kwenye akaunti ya mteja kutokana na maelekezo
yake.

Benki ilijiridhisha kuwa malipo yote
yaliyofanywa kutoka kwenye akaunti ya VIP
ni halali kwa kuwa chanzo cha pesa hizo
ilikuwa ni halali kutokana na mauzo ya
hisa na ulipwaji wa kodi ya Serikali kama
ilinyoelezwa hapo juu. Kutokana na sababu hiyo benki haikuwa na shaka juu ya malipo hayo.

4.3 Malipo taslimu kwa wateja na kubeba fedha kwenye viroba, mifuko ya rambo na magunia
Benki inatoa tamko kuwa malipo yote
yaliyofanywa katika akaunti ya VIP
yalilipwa kupitia akaunti za walipwaji.
Hakuna fedha zilizolipwa taslimu kwa
wateja na kubebwa kwenye viroba au
magunia kama ilivyoripotiwa Bungeni. Pesa
iliyotoka kwenye akaunti ya VIP tarehe 6
Februari, 2014 kiasi cha shilingi
3,314,850,000.00 ililipwa kwenye akaunti
nane za wateja tofauti na siyo kubebwa
kwenye viroba au magunia.
Na zile zilizotoka toka benki ya Stanbic
zilizotajwa hapo juu zilitumwa kwa njia ya TISS na siyo kubeba kwenye magunia au viroba.

4.4 Malipo kwa mfanyakazi wa benki ya
Mkombozi Gazeti la Mawio la tarehe 20-26, Novemba, 2014 tolea namba 0122 liliandika kuwa mwanasheria wa benki ya Mkombozi ajulikanaye kwa jina la Rweyengeza Alfred alipokea malipo toka akaunti ya VIP ya shilingi milioni 40.2.

Benki inatoa tamko kuwa haina mfanyakazi anayetambuliwa kwa jina hilo na wala hakuna mfanyakazi yeyote wa benki aliyelipwa fedha toka kwenye akaunti ya VIP.

Wito kwa umma
Benki ya Mkombozi inachukua fursa hii
kuwatarifu wateja wake na umma
kutopotoshwa na taarifa au tuhumma
zilizofafanuliwa hapo juu na kuwataka
wateja wake wote kutokuwa na hofu yeyote
kwani benki ipo imara na inafanya kazi
kwa kufuata misingi ya sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa na Benki Kuu ya
Tanzania. Benki inawataarifu wateja wake na Watanzania kwa ujumla kutoyumbishwa
na tuhumma hizo ambazo hazina ukweli
ndani yake na badala yake waitumie benki yao kwa shughuli za maendeleo ya nchi yetu.

Pamoja tunajenga nchi na uchumi wa nchi yetu. Hitimisho Benki ya biashara ya Mkombozi haijihusishi na haitajihusisha na utakasishaji wa fedha
chafu.




Imetolewa na:
MKURUGENZI MTENDAJI BENKI YA
BIASHARA YA MKOMBOZI

Chapisha Maoni

 
Top