BWANA KHALIST LUANDA AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA
HABARI (HAWAPO PICHANI) JUU YA
KUKAMILIKA KWA MAANDALIZI YA
UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA
MJINI DODOMA LEO AMBAPO ALITANGAZA RASMI TAREHE YA
KUANDIKISHA KUPIGA KURA .
(PICHA NA HABARI KUTOKA OFISI YA WAZIRI MKUU TAMISEMI).
====== ========
Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa katika
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali Mitaa Bwana Kharist Michael
Luanda amesema wananchi wanapaswa
kujiandikisha katika daftari maalum la
kupigia kura kwa ajili ya kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuanzia tarehe 23/11/2014 hadi tarehe 29/11/2014.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa wananchi wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika ngazi za vijiji, vitongoji na mitaa wanapaswa kuchukua fomu za kugombea kuanzia tarehe 16/11/2014 hadi tarehe 22/11/2014. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, Bwana Luanda aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi la kujiandikisha ili
waweze kupata fursa ya kushiriki katika
kupiga kura ili kuwachagua viongozi wa
vijiji, vitongoji na mitaa wanaowataka.
Alisema sifa za mtu anayestahili
kujiandikisha kushiriki uchaguzi huo ni
lazima awe raia wa Tanzania, mwenye
umri wa miaka 18 au zaidi, mkazi wa eneo
hilo na mwenye akili timamu.
Pia alisisitiza kuwa uandikishaji huo
utafanyika katika vituo maalum
vilivyoandaliwa ambavyo vipo katika
majengo ya umma, isipokuwa sehemu
ambazo hazina majengo hayo, uandikishaji utafanyika katika vituo maalum kutokana na makubaliano ya Msaidizi wa Uchaguzi
na viongozi wa vyama vya siasa.Bwana
Luanda amesisitiza kuwa vituo hivyo
vitafunguliwa saa 1:30 asubuhi na
kufungwa saa 10:30 jioni.
Aidha alisema kuwa vyama vya Siasa
vitaruhusiwa kuweka mawakala wao
wakati wa uandikishaji wa wa wapiga kura
lakini gharama za kuwalipa zitakuwa juu
ya chama husika. Kuhusu sifa za mtu
anayetaka kugombea nafasi mbalimbali
katika ngazi ya vitongoji, vijiji na mtaa
Mkurugenzi huyo alisema kuwa ni lazima awe mtanzania mwenye umri wa miaka 21 au zaidi na awe mkazi wa kudumu wa eneo husika.
Vile vile alisema kuwa wasimamizi
wasaidizi wa kila kituo wanapaswa
kubandika orodha ya wapiga kura tarehe
30/11/2014, endapo mkazi yeyote au chama cha siasa kitakuwa na pingamizi au maoni juu ya orodha hiyo basi awasiliane na msimamizi msaidizi wa uchaguzi ili kuweza kufanyia marekebisho na orodha ya mwisho
itabandikwa siku tatu kabla ya uchaguzi.
Uchaguzi wa serikali za Mitaa Tanzania
Bara umepangwa kufanyika disemba 14,
2014, ambapo wananchi watawachagua wenyeviti wa vijiji, vitongoji, Mitaa, Wajumbe wa Halmashauri za vijiji na
Wajumbe wa Kamati za Mitaa.
Viongozi watakaochaguliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa ni pamoja nabwajumbe wa Halmashauri ya Kijiji
wasiopungua 15 na wasiozidi 25, wenyeviti wa Mitaa na wajumbe wa kamati za Mitaa wasioziidi 6 na wenyeviti wa vitongoji wa
kila kitongoji.
Chapisha Maoni