0
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya
ndani ya nchi Bw. Mbaraka Abdualwakil,
Mwakilirishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano Sayansi na Teknolojia
ambaye ni Mkurugenzi wa utawala na
rasilimali watu, Bi Selina Lyimo wakiwa
Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi
Abdulrahaman Kaniki pamoja
makamishina wa Jeshi la Polisi wakati wa hafla ya makabidhiano ya chapisho la utafiti wa tathmini ya Polisi jamii . Picha na Alexander Mpeka – Jeshi la Polisi.
======= ======= =======

Na. Tamimu Adam - Jeshi la Polisi.

Jeshi la Polisi nchini limetakiwa kutumia
matokeo ya utafiti wa tathmini ya Polisi
Jamii uliofadhiliwa na Wizara ya
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kupitia
Tume ya taifa ya Sayansi na teknolojia
( COSTECH) katika kuboresha mkakati wa
Polisi jamii ili kuimarisha ulinzi na
usalama wa raia na mali zao kwani
matokeo hayo yana manufaa makubwa
katika kubaini, kuzuia, na kutanzua
uhalifu na kero mbalimbali katika jamii.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa
Utawala na Rasilimali watu Bi. Selina
Lymo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa
Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na
teknolojia wakati wa hafla ya kukabidhi
chapisho la utafiti wa matokeo ya
tathmini ya Polisi jamii nchini kwa Katibu
Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya
nchi Bw. Mbaraka Abdulwakili .
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara
ya Mambo ya ndani ya nchi Bw. Mbaraka
Abdulwakili alisema atahakikisha utafiti
huo unafanyiwa kazi ipasavyo na
amewataka watendaji wa Jeshi la Polisi
kutumia utafiti huo katika kuimarisha
usalama wa raia na mali zao kwa kuwa
askari waliopo hawatoshi na Polisi jamii
imeonyesha mafanikio makubwa katika
kuzuia vitendo vya uhalifu na wahalifu.
Naye, Mtaalum Mwelekezi wa Utafiti wa
Tathmini ya Polisi Jamii ambaye pia ndiye
Mtafiti Mkuu Dkt Haji Semboja alisema
kuwa utafiti huo ulifanyika katika kanda
saba ambapo matokeo ya utafiti huo
yanaonesha kuwa uhusiano wa kiutendaji baina ya wananchi na Jeshi la Polisi umeboreshwa kwa kiwango kikubwa kupitia
dhana ya Polisi jamii.
Alisema kuwa jambo hilo linasaidia katika kutengeneza mazingira ya amani na hivyo
shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii
zinaweza kuendelea kufanyika bila hofu na
kwa uhakika wa ulinzi na usalama.
Aliongeza kuwa, utafiti huo umeonyesha
kwamba, watu wengi wanaamini kuwa,
matokeo ya kuanzishwa kwa Polisi jamii
katika maeneo yao kuna mafanikio
makubwa katika kuhimiza na kutia moyo
uvumbuzi wa njia mpya za kukabiliana na
vitendo vya uhalifu ambapo wananchi
wamekuwa wakihimizwa utoaji wa taarifa za uhalifu kupitia njia mbalimbali ikiwemo njia ya ujumbe mfupi.

Naye, Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi,
Abdulrahman Kaniki aliipongeza timu
nzima iliyofanya utafiti huo na kusema
kuwa Jeshi la Polisi kama watekelezaji
wakuu wa Programu ya maboresho
yaliyojikita katika mihimili mikuu mitatu
ambayo ni Weledi, Usasa na Polisi jamii,
wanatambua na kuthamini kazi nzuri
iliyofanywa na watafiti hao na
amewaomba kuangalia namna
wanavyoweza kufanya utafiti katika
mihimili mingine miwili iliyobaki ambayo
ni Usasa na Weledi ili Jeshi Polisi liweze
kuwa na tathimini halisi ya Maboresho
yake.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa
Mkurugenzi mkuu wa Tume ya Taifa ya
Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dr. Flora
Tibazarwa alisema kuwa madhumuni ya
mpango wa utafiti huo yalikuwa ni
kuimarisha uhusiano baina ya Jeshi la
Polisi na wananchi katika kuzuia na
kutatua matatizo ya jamii, msisitizo ukiwa
kuzuia uhalifu kabla haujatokea.
Aliongeza kuwa matokeo ya utafiti huo
yatawasaidia watunga sera na watoa
maamuzi kutoa maamuzi na kutunga sera mbalimbali za usalama wa raia na mali zao kwa faida ya taifa letu.

Chapisha Maoni

 
Top