0
MKUU wa Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara, Festo Kiswaga amewasweka rumande watendaji 17 wa vijiji na kupewa barua za onyo kali, huku
mmoja akifukuzwa kazi kwa uzembe wa
kutosimamia ipasavyo ujenzi wa maabara za shule za sekondari.

Hali hiyo ilitokea katika ziara aliyoifanya kujionea maendeleo ya ujenzi wa maabara hizo, ambazo Rais Jakaya Kikwete alitoa maagizo kwa wakuu
wa wilaya zote nchini kusimamia ujenzi wake katika shule zote za kata na ukamilike hadi ifikapo Novemba 30, mwaka huu.

“Siwezi kukubaliana na uzembe wa watendaji hawa wa vijiji, kabla mimi sijafungasha virago kwenda kwetu, kwanza nawashughulikieni ninyi ili
muweze kusimamia vizuri maagizo ya serikali na mkilala siku moja rumande, mtakuwa mmetafakari nini cha kufanya na kama kazi imekushinda,
andika barua ya kuacha kazi mara moja,” alisema Kiswaga.

Alisema suala la ujenzi wa maabara nchini halina masihara, hivyo kila mtendaji wa serikali na mwananchi wa kawaida, wawajibike ipasavyo ili
watoto wao wasome vizuri masomo ya sayansi nchi ipate wataalamu katika fani mbalimbali za sayansi.

“Ujenzi huu utawanufaisha watoto wetu sisi wenyewe kwa nini sasa tusukumame kwa kiasi hiki huu ni wimbo wa nchi nzima utake utaimba
usitake utaimba sasa tushirikiane kwa pamoja ili kumaliza ujenzi kwa usalama kabisa,” alisema.

Watendaji walioswekwa rumande ni wa vijiji vya Mkumbaru, Amani, Mara, Sengenya, Mpombe, Chimika, Msinyasi, Kismatuli, Nachura na
Misawaje.

Mtendaji aliyefukuzwa kazi kutokana na kutoshiriki masuala ya serikali kwa muda mrefu ni wa kijiji cha Changwale katika kata ya Lumesele.

Chapisha Maoni

 
Top