Atamba hababaikii vyeo, aliyetoa
Siku tatu baada ya Rais Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka, mwanasiasa huyo ametua jimboni kwake na kupokelewa kwa mbwembwe na wananchi wa
jimbo hilo huku akisema hajutii kung’olewa.
Jumatatu wiki hii, Rais Kikwete akihutubia Taifa kupitia mkutano wa wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, alitangaza kumvua nafasi ya uwaziri Prof.
Tibaijuka kutokana na kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow ambayo yeye (Tibaijuka) alipata mgawo wa Sh. bilioni 1.6 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji
wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing LTD, James Rugemalira.
Prof. Tibaijuka ambaye ni Mbunge wa Muleba Kusini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliwasili jimboni mwake juzi ikiwa ni siku moja baada ya kutimuliwa katika wadhifa wake na
kupokelewa na wapigakura wake ambao
walimuahidi kumpa ushirikiano wakati akitekeleza majukumu yake jimboni akiwa mbunge.
ALIVYOPOKEWA
Profesa Tibaijuka aliwasili mjini Bukoba kwa ndege na kupokelewa na mamia ya wananchi na msafara wa mapokezi ulianza kuondoka katika uwanja huo saa 7:00 mchana kuelekea kijijini kwake Kagabiro, wilayani Muleba.
Msafara huo ulikuwa na magari zaidi ya 35 na pikipiki 50 yaliyowabeba wapambe, wakereketwa na wanachama wa CCM.
Wakati wa msafara huo, wananchi hao walikuwa wakiimba nyimbo za kumsifu Prof. Tibaijuka wakisema “ni jembe”.
Msafara uliwasili kijijini kwa Prof. Tibaijuka saa 10: 00 jioni na wananchi waliohudhuria hafla ya kumpokea kutoa salamu wakimtakia afya njema
na kumuomba kuwa mvumilivu kwa yote
yaliyojitokeza kutokana na kuvuliwa uwaziri.
Wananchi hao walimweleza Prof.Tibaijuka kuwa licha ya Rais Kikwete kumvua uwaziri, lakini wao
wana imani naye katika kuwaletea maendeleo jimboni humo.
“Mheshimiwa Mbunge, sisi wananchi wa jimbo lako bado tuna imani nawe, tupo tayari kukupa ushirikiano kuhakikisha unatekeleza vyema yale yote uliyoyapanga kuwaletea wanaMuleba,”
alisema Josephat Rweyemamu wakati
akizungumza kwa niaba ya wananchi.
Rweyemamu alisema kuwa wananchi wa jimbo hilo walimchagua Prof. Tibaijuka kuwa mbunge wao, hivyo kuvuliwa nafasi ya uwaziri haiwapi
tabu kwani hizo ni nafasi za ziada kwa kiongozi yeyote.
Naye Alhaji Shakiru Kyetema, alisema Prof. Tibaijuka hana sababu ya kusikitika kutokana na kuvuliwa uwaziri kwani kuanzia sasa atapata muda mzuri wa kuwatumikia wapiga kura wake
tofauti na alipokuwa waziri.
Aidha, wananchi hao walimzawadia Prof.Tibaijuka zawadi mbalimbali akiwamo ng’ombe dume aliyetolewa na Alhaji Shakiru kama ishara ya kumpongeza kwa msimamo wake kama kiongozi mwanamke.
ATEMA CHECHE
Prof. Tibaijuka akizungumza na wananchi hao, aliwataka wasisikitike kwa kuvuliwa kwake nafasi ya uwaziri kwani aliyetoa ndiye aliyetwaa.
Alisema binafsi hajutii kuvuliwa cheo hicho kwani kama angekuwa na tamaa ya cheo asingetoka Umoja wa Mataifa (UN) ambako alilazimika kuacha
cheo ili akawatumikie wananchi wa jimbo la Muleba.
“Najua wengi wenu mmeumizwa na masuala ya sakata la Escrow, niwaombe yasiwaumize vichwa kwani Bwana alitoa na Bwana ametwaa. Jina lake
lihimidiwe,” alisema Prof. Tibaijuka.
Prof. Tibaijuka alisema kimsingi, suala la yeye kupokea fedha kutoka kwa James Rugemalira halina utata kwani fedha hizo zilitolewa kuwasaidia kuwalipia karo baadhi ya wanafunzi wanasoma kwenye shule zake, hivyo hawezi kuwa
mbinafsi kama ilivyotafsiriwa na baadhi ya Watanzania.
“Watanzania tumejaa ubinafsi, kila mtu anafikiria kila anafanya jambo anategemea kupata posho, na niwahakikishieni mimi sina uchu wa ubinafsi wala tamaa za vyeo kwani kama ni cheo nilichoacha UN kilikuwa kikubwa zaidi,” alisema akimaanisha ni cha ukamishna mkuu wa makazi.
Aliwahakikishia wananchi hao kuwa kwa sasa nguvu zake anazirudisha jimboni na kila mwananchi atatambua kuwa yeye ni nani kwani atahakikisha muda uliobaki jimbo lake linainuka kimaendeleo kuanzia kata kwa kata hususani katika sekta ya elimu.
Aidha, aliwahadharisha watu wanaonyemelea jimbo lake kwa kuwaambia wakae chonjo.
Kabla ya kuvuliwa uwaziri, Alhamis iliyopita Prof. Tibaijuka aliitisha mkutano wa waandishi wa habari ghafla na kusema hawezi kujiuzulu. Prof. Tibaijuka alisema kamwe hawezi kujiuzulu
na pia anajivunia na kuona fahari kupata fedha hizo. Kampuni hiyo ya Rugemalira ilikuwa mwana hisa katika IPTL.
Alisema ni bora alivyopata fedha hizo na
kuzipeleka katika shule yake kwa ajili ya kusaidia shughuli za elimu kwa watoto wa kike wasio na uwezo.
Kutokana na hali hiyo, alisema anahitaji kusifiwa kwa ujasiri wake wa kukiri kupokea fedha hizo na kuzitolea maelezo, ingawa alikosa nafasi hiyo
katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Alisema angejiuzulu iwapo ingethibitika fedha hizo za Rugemalira, siyo halali.
Prof. Tibaijuka alisema fedha hizo
hazijathibitishwa na serikali kuwa siyo halali, kiasi cha yeye kutakiwa kujiuzulu nafasi yake serikalini.
Alisema fedha hizo hazina uhusiano kati yake na nafasi ya uwaziri aliyonayo, kwani zilikwenda moja kwa moja kusaidia kulipa deni la Sh. bilioni 2,
ambazo moja ya shule zake ilikopa kutoka Benki M.
Prof. Tibaijuka alisema iwapo itabainika fedha hizo si halali atakuwa tayari kuzirudisha. “Iwapo fedha hizo zitathibitika siyo halali, Joha
Trust itazirudisha, kama taasisi inavyoitwa nia njema, sisi hatuhifadhi fedha zisizo halali,” alisema Prof. Tibaijuka.
Alisema fedha hizo alizipokea Februari 12, mwaka huu, zilitokana na maombi ya awali kutafuta michango kutoka kwa wafanyabiashara wa ndani
na wafadhili wa nje.
Alisema hoja kwamba, alipokea mchango mkubwa, haina uzito kutokana aina ya mtu, ambaye alimpaa mchango huo na kusema ni mtu mwenye fedha na pia ni mfanyabiashara.
“Labda mnafikiri unapoomba fedha kwa mtu kama Bill Gates unategemea atakuchangia kama kiasi gani? Siyo senti.
Hata mimi nilipoambiwa na Rugemalira
nikaangalie akaunti yangu ina shilingi ngapi nakukuta fedha nyingi, nilijua leo nimeamkia mkono wa kulia. Nilifurahi,” alisema Prof. Tibaijuka.
Alisema fedha hizo alichangiwa kwa ajili ya kulipa sehemu ya deni la Sh. bilioni mbili anazodaiwa na Benki M baada ya kukopa kwa ajili ya ujenzi wa bweni la shule lenye uwezo wa vitanda 163.
Alisema fedha hizo zimechangia maendeleo ya elimu kwa kuwatengenezea wanafunzi mazingira
bora.
“Hii kitu inabidi tuwe makini kama Taifa, kwani mimi nilikuwa mtumishi Umoja wa Mataifa. Lakini sikuweza kubeba fedha. Na kuna mapesa kule.
Iwe katika nchi hii, ambayo nafahamu hata wapigakura wangu wa kule Muleba Kusini na wakulima wanaishi maisha ya chini?” alihoji Prof.
Tibaijuka.
Alisema uamuzi wa kuzitoa fedha hizo haraka katika Benki ya Mkombozi, ulifikiwa na Bodi ya Wadhamini ya Joha Trust, ambayo ilitoa maamuzi kwamba, zitumike kulipa deni la Benki M.
Hata hivyo, katika mkutano huo Prof. Tibaijuka hakutoa nyaraka zozote zikiwamo risiti zinazoonyesha deni hilo lilivyolipwa kupitia benki
hiyo.
Prof. Tibaijuka alisema analazimika kutoa maelezo hayo katika vyombo vya habari kutokana na kutopewa nafasi ya kufanya hivyo mbele ya PAC.
Alisema serikali bado haijathibitisha kuwa fedha za Rugemalira ni haramu kiasi cha yeye kulaumiwa.
Kutokana na hali hiyo, alionya kuwa kujiuzulu kusiwe kama mtindo, kwani fedha hizo hazikugusa utendaji kazi wake kama mtumishi wa
serikali.
Alisema mitandao inaendelea kuandika na asilimia kubwa wakimtukana.
Africa Newss
CHANZO: NIPASHE
Chapisha Maoni