0
Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira Miguu nchini ‘TFF’, imeahidi kuendesha uchaguzi mkuu wa Shirikisho hilo kwa Kufuata Uhuru na Haki na kuzingatia taratibu, kanuni na sheria zote zilizopo, huku wakipinga kabisa vitendo vya Rushwa katika kipindi chote cha uchaguzi huo.
Mwenyekiti wa Kamati Hiyo, Wakili Revocatus Kuuli, amesema kwamba kamati yake haitakuwa na huruma kwa ishara yoyote ya rushwa katika kipindi chote cha uchaguzi n kwamba itafanya kazi na Taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na jeshi la Polisi kuhakikisha uchaguzi huo hautakuwa na vitendo vya rushwa.
-Tunawatahadharisha wagombea wote kukaa mbali na vitendo vya rushwa, kamati yetu haitakubali vitendo hivyo na tutafanya kazi na mamlaka za Serikali kuhakikisha yeyote atakayehusika na vitendo hivi anachukuliwa hatua, TAKUKURU wataufuatilia kwa karibu uchaguzi huu,” alisema Kuuli.
Ratiba ya Uchaguzi.
Akizungumzia mchakato mzima, Kuuli amesema, mchakato wa kuchukua fomu na kuzirejesha utaanza Juni 16 hadi Juni 20 Mwaka huu na kikao cha mchujo wa awali kwa wagombea kitafanyika Juni 21 mkapa Juni 23.
Aidha kuanzia Juni 24 na 25, mwaka huu, kamati itafanya kazi ya kuchapisha na kubandika kwenye mbao za matangazo majina ya wagombea wakati Juni 26 hadi 28 zitakuwa siku za kupokea na kuweka mapingamizi kwa wagombea na Juni 29 mpaka Julai Mosi itakuwa kipindi cha kupitia mapingamizi yote na kufanya usaili.
Kwa mujibu wa Kuuli, Julai 2 mpaka 3 kitakuwa kipindi cha kuchapisha na kubandika matokeo ya usaili, wakati Julai 4 hadi 7 na kipindi cha Sektretarieti kuwasilisha masuala ya Kimaadili kwenye Kamati ya maadili, ambapo Julai 7 hadi 11 ni kipindi cha kusikiliza na kutolea maamuzi masuala ya kimaadili.
Ratiba pia inaonesha kuwa
Julai 15 hadi 17 kitakuwa ni kipindi cha kukataa Rufaa kwa maamuzi ya masuala ya kimaadili kwenye kamati ya rufaa ya Maadili ya TFF, na
Julai 18 hadi 22 itakuwa siku ya kusikiliza rufaa za maadili na Julai 23 mpaka Julai 25 itakuwa siku ya kutoa maamuzi ya Rufaa.
Julai 26-28 kitakuwa kipindi cha kukata rufaa dhidi ya kamati ya Uchaguzi kwenye Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF, rufaa hizo zitasikilizwa Julai 29 mpaka Agosti 2, ambapo Wagombea watajulishwa matokeo ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF na Agosti 5 hadi 6 itakuwa siku ya kuchapisha majina ya wagombea watakaoingia kwenye Uchaguzi huo.
Kampeni kwa wagombea zitaanza Agosti 7 mpaka 11 na siku inayofuata yaani Agosti 12 itakuwa siku ya uchaguzi wa viongozi wa TFF.
Aidha Wakili Kuuli amewaambia waandishi wa habari kuwa Nafasi zinazogombewa ni Rais wa TFF, Makamu wa Rais pamoja na nafasi 13 za wajumbe TFF wanaowakilisha kanda 13 za Kagera na Geita, Mara na Mwanza, Shinyanga na Simiyu, Arusha na Manyara,
Kigoma na Tabora, Katavi na Rukwa, Mbeya na Iringa, Njombe na Ruvuma, Lindi na Mtwara, Dodoma na Singida;, Pwani na Morogoro,
Kilimanjaro na Tanga pamoja na Dar es Salaam ambayo ni kanda pekee.

Chapisha Maoni

 
Top