0
Mtoto Nuru Mohamedi (7) ameuawa kikatili na kisha mwili wake kutelekezwa kwenye nyumba ambayo haijakamilika ujenzi iliyo Majohe Kichangani jijini Dar.

Tukio hilo, ambalo limezua hofu na huzuni kwa wakazi wa mtaa huo, lilibainika jana baada ya kupatikana kwa maiti ya mtoto huyo ambaye kabla
ya mauti kumkuta alikuwa amepotea katika mazingira ya kutatanisha tangu Novemba 6.

Akisimulia tukio hilo kwa tabu huku akilia kwa huzuni, mama mzazi wa mtoto huyo, Sauda Ally alisema Alhamisi iliyopita saa 1:00 usiku mtoto
wake alikuwa akicheza nje ya nyumba yao pamoja na watoto wengine wawili.

“Baadaye akaja mtoto wa jirani aitwaye Dula, akaniambia Nuru amekwenda na babu mmoja alimwambia amsindikize dukani, nilinyanyuka haraka na kutoka nje na kuanza kumwita, lakini
hakuitika,” alisema.

Alisema baada ya kuona hali hiyo alikimbia hadi dukani alikoelekezwa kuwa mwanaye amekwenda,
lakini hakumwona hivyo aliamua kuomba msaada kwa majirani na taarifa zilipelekwa katika msikiti wa karibu kwa ajili ya kutangazwa na kisha waliendelea kutoa taarifa hizo kituo cha polisi cha
Gongo la Mboto.

Alisema mtoto wake alitafutwa bila mafanikio kwa siku sita.
Alisema, jana asubuhi mmoja wa wapangaji wake alipokea simu kutoka kwa jirani yake anayeishi eneo la Kwa Mkandawile kwamba kuna maiti ya
mtoto imeonekana katika maeneo hayo na kwamba huenda akawa ni mtoto wake.

Hata hivyo, Sauda alishindwa kuelezea zaidi mkasa huo na mama mkubwa wa marehemu, Rehema Ally alisema kuwa baada ya simu hiyo waliondoka mara moja kwenda eneo la tukio.

“Tuliona maiti ya mtoto ikiwa imefukiwa kwa matofali na sehemu ya kichwa ikiwa imebaki nje”. “Kwa kweli hali tuliyoikuta ilikuwa inatisha. Alikuwa amefunikwa kwa matofali, upande wa
kisogoni tu ndiyo ulikuwa ukionekana. Tulitoa taarifa polisi na walipofika, waliinyanyua na ndipo tulipothibitisha maiti ile ilikuwa ya Nuru na
alikuwa amevuliwa nguo zote.”
Alisema watekelezaji wa tukio hilo walifanya ukatili wa hali ya juu, kwani baada ya uchunguzi wa
daktari ilibainika kuwa na majeraha katika sehemu ya paja, lililokuwa na tundu lililofunikwa kwa
plasta na kisogoni ilionekana amepigwa na kitu kama jiwe.

Alisema anasikitishwa na kitendo cha kuuawa kinyama na kudhalilishwa alichofanyiwa mtoto wao, kwani kinaonyesha kushuka kwa hali ya
usalama wa watoto na kuitaka polisi kuhakikisha inachunguza kwa undani taarifa za utekaji watoto
na si kuzipuuzia.

Aliongeza kuwa maiti ya mtoto wao walitarajia kuizika jana baada ya taratibu za kipolisi kukamilika.
Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa eneo hilo walipeleka lawama zao kwa polisi kwa kukanusha taarifa za utekaji watoto pasipo kuzifanyia uchunguzi wa kina.

Mkazi mwingine, Zena Ramadhani alisema kupotea kwa Nuru ni tukio la pili kwa eneo hilo ndani ya mwezi mmoja na mtoto wa kwanza kupotea hajaonekana hadi leo.
“Hivi sasa tunaishi na watoto wetu kwa shaka, japo polisi wanasema hakuna utekaji nyara, sisi kama wazazi hatukubaliani na hilo kwa sababu
nimeshuhudia na hili ni tukio la pili. Sasa
utaniambiaje kuwa taarifa hizo ni za uongo.” Alipotafutwa Kamishna wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alikataa kuzungumza
moja kwa moja na kusema atafutwe Kamanda wa Ilala, Mary Nzuki.

Hata hivyo, Kamanda Nzuki alipopigiwa simu zaidi ya mara tano hakupokea na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno kuhusiana na tukio hilo,
hakujibu.
Ustadhi wa msikiti katika eneo hilo, Jumanne Hamis ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM Mtaa wa Kichangani, aliyetoa tangazo la kupotea kwa mtoto msikitini kwa mara ya kwanza alisema amesikitishwa mno na taarifa za kifo cha mtoto
huyo.

“Kwa kweli siamini kilichotokea na kama kuna binadamu anayeweza kufanya jambo hilo kwa mtoto wa miaka saba.”

Chanzo: Mwananchi

Chapisha Maoni

 
Top