0
Bibi Mariam Abdallah, mwenye umrin wa miaka 60, mkazi wa Kijiji cha Mnanila, ambaye anadaiwa kushushiwa kipigo nyumbani kwake na Askari wa
JWTZ,akiwa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma, Maweni kwa matibabu.

Akielezea mkasa huo Mariam Abdallah alisema kuwa Novemba 23 mwaka huu, majira ya saa tatu usiku, watu wanne waliokuwa wamevalia sare za
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), walivamia nyumbani kwake wakimtafuta mwanamke aliyejulikana kwa jina moja la Editha, ambaye anadaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mmoja wa wanajeshi hao ambaye hakufahamika
mara moja jina lake.

Inadaiwa kuwa siku moja kabla, askari huyo wa JWTZ, alikuwa amegombana na mpenzi wake huyo, ugomvi uliosababisha askari huyo kung’atwa kidoleni na mpenzi wake ambaye
baada ya kitendo hicho alimtoroka, ambapo siku iliyofuata aliamua kumtafuta hadi kwa bibi Mariam
anaedaiwa kuwa ndugu wa mwanamke huyo.

Hata hivyo baada ya kufika nyumbani kwake bibi huyo aliwajibu kuwa hakuwa anafahamu alipo mwanamke huyo, lakini cha kushangaza mmoja wa askari jeshi hao alianza kumshushia kipigo
mfululizo kwa mateke na ngumi na kumjeruhi sehemu mbali mbali za mwili wake hasa maeneo ya usoni na kumsababishia maumivu makali kiasi
cha kulazwa hospitali.

“Walikuwa wanajeshi wanne, ila hao wengine hawakunigusa mmoja ndiye alinipiga nikiakimbilia jikoni lakini alinifuata hadi jikoni,” alisema Mariam.

Ofisa Muuguzi katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Kigoma, Maweni, Siyaleo Shilambele, alisema majeruhi huyo ameumia sana sehemu za usoni
kiasi ambacho jicho lake moja lilikuwa likitoa usaha na hawezi kuona vizuri.

“Bado tunaendelea na uchunguzi wa kumfanyia vipimo mbali mbali na kumpa matibabu ya awali na pia tumempiga picha za X-ray kichwani ili kuona mifupa ya usoni iliumia kiasi gani,” alisema
ofisa muuguzi huyo.

Mamlaka za polisi hazikuweza kupatikana kuzungumzia tukio hilo ambapo imeelezwa kuwa wakuu wa kipolisi wa mkoa wa Kigoma, wako
nchini Burundi kwenye ziara ya ujirani mwema.

Chapisha Maoni

 
Top