0
Pamoja na Kushiriki Vikao vya Bodi, CAG alipata nafasi ya kufika katika Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa ambako alipokelewa na Mwenyeji wake, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Balozi Ramadhani Mwinyi. Akiwa katika Uwakilishi wa Kudumu CAG alijionea maendeleo ya ukarabati wa Jengo la Uwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Profesa Mussa Juma Assad
ameelezea kuridhishwa kwake na mwenendo wa vikao vya Bodi ya Wakaguzi ya Umoja wa Mataifa ( UNBoA) na kuahidi
kushirikiana na kufanya kazi kwa karibu na wajumbe wenzie wanaounda bodi hiyo.

Ameyasema hayo siku ya jumanne wakati wa wajumbe wa Bodi hiyo walipokutana hapa Umoja wa Mataifa. 

Hii ni mara ya kwanza kwa CAG kuhudhuria vikao vya Bodibhiyo ambayo wajumbe wake ni wadhibiti na
wakaguzi wakuu wa hesabu za serikali
kutoka Uingereza, Tanzania na India
Profesa Mussa Juma Assad ambaye
ameteuliwa hivi Karibu na Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali akichukua
nafasi ya Bw. Ludovick Utouh ambaye
amestaafu kwa mujibu wa sharia,
amewaeleza wajumbe wenzie kuwa
amejifunza mengi.
Katika kikao chao cha siku moja
kilichotanguliwa na kikao cha jopo la
wakaguzi wa nje kilichojadilia taarifa
mbalimbali za mashirika ya Umoja wa
Mataifa ikiwamo taarifa ya Shirika la
Kimataifa la Nguvu za Atomic, wajumbe wa
Bodi walijadiliana pamoja na mambo
mengine changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao kama wakaguzi wa hesabu za Umoja wa Mataifa.

Awali wakizugumza kwa nyakati tofauti,
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kutoka Uingereza Bw.Amyas Morse na Bw. Shashi Sharma
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kutoka India
pamoja na kumkaribisha Profesa Assadi
katika Bodi hiyo pia walimuahidi
ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu waliyokabidhiwa.

Aidha katika kikao hicho cha Bodi ilitolewa taarifa kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kutoka Tanzania ( CAG) atashika uenyekiti wa Bodi kuanzia Januari Mosi mwakani.

Nafasi hiyo ya uenyekiti huwa ni ya
mzunguko wa kipindi cha miaka miwili
ambapo hivi sasa inashikiliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kutoka Uingereza.

Aidha Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Nje, Bw. Fransis Kitauli ambaye ndiye
anayemwakilisha CAG katika utekelezaji wa mukumu ya kila siku ndani ya Bodi hiyo naye atakuwa mwenyekiti wa Kamati ya Operesheni za Ukaguzi ( AOC)
Bodi ya Ukaguzi wa Umoja wa Mataifa, ni chombo huru na kinachojitegemea chenye
jukumu la kukagua vitabu vya hesabu za
Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa,
Mashirika na Taasisi zote zilizochini ya
Umoja wa Mataifa, Misheni za Ulinzi wa
Amani za Umoja wa Mataifa na Miradi
mbalimbali inayosimamiwa na Umoja wa Mataifa.

Tanzania kupitia Ofisi ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
ilichaguliwa kuwa Mkaguzi wa Hesabu za Umoja wa Mataifa mwaka 2012 ikichukua nafasi ya Afrika ya Kusini. 

Aidha Tanzania ambayo itadumu katika Bodi ya Wakaguzi ya Umoja wa Mataifa kwa Miaka sita inakuwa nchi ya Tatu ya Afrika kushika wadhifa huo nyeti ikitanguliwa na Ghana na Afrika ya Kusini.

Chapisha Maoni

 
Top