Wenyeviti watatu wa Kamati za Bunge waliopendekezwa kuwajibishwa na Bunge hilo katika sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow wataondolewa katika nyadhifa zao ndani ya siku 21 zijazo, imeelezwa.
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai
alisema jana kuwa utekelezaji wa
maazimio ya Bunge kwa upande wa
mhimili huo wa dola utafanyiwa kazi
mapema mwakani.
“Hilo litatekelezwa wakati wa Kamati za
Bunge ambazo zitaanza mwishoni mwa
wiki ya pili ya Januari mwakani kwa
kamati husika kuchagua wenyeviti
wapya.”
Wenyeviti hao ni wa Kamati ya Nishati
na Madini, Victor Mwambalaswa,
William Ngeleja wa Katiba, Sheria na
Utawala na Andrew Chenge wa Kamati ya Bajeti.
Tuhuma zao Chenge ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi (CCM) alitajwa katika ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuwa aliwekewa Sh1.6 bilioni katika akaunti yake binafsi kama ilivyokuwa kwa Ngejela (Sengerema -
CCM) ambaye aliingiziwa Sh40.4 milioni.
Wote waliingiziwa fedha hizo na mmiliki
wa Kampuni ya VIP Engineering &
Marketing, James Rugemalira.
Mwambalaswa, ambaye pia ni Mbunge
wa Lupa (CCM), ametajwa kwa kuwa
alikuwa makamu mwenyekiti wa Bodi ya
Tanesco ambayo Bunge liliazimia kuwa
wajumbe wake wawajibishwe.
Katika azimio namba tatu, Bunge
lilielekeza kuwa kamati husika za
kudumu za Bunge zichukue hatua za
haraka na kwa vyovyote vile kabla ya
Mkutano wa 18 wa Bunge, kuwavua
nyadhifa zao wenyeviti tajwa wa kamati
husika za kudumu za Bunge.
Utekelezaji wa azimio hilo unakuja baada ya Serikali kuanza kuwawajibisha vigogo wake waliotajwa katika ripoti hiyo.
Jumatatu iliyopita, Rais Jakaya Kikwete
alimfukuza kazi, Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Profesa Anna Tibaijuka ambaye kama
ilivyokuwa kwa Chenge na Ngeleja,
aliingiziwa Sh1.6 bilioni katika akaunti
yake binafsi kinyume na kanuni za
maadili ya viongozi wa umma.
Pia, wakati Rais Kikwete akimuweka
kiporo Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo, juzi Katibu
Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue
alimsimamisha kazi, Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini, Eliakimu
Maswi kupisha uchunguzi wa tuhuma
dhidi yake.
Hao wote walitanguliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema ambaye alijiuzulu kutokana na kashfa hiyo akisema ushauri wake haukueleweka hivyo kuchafua hali ya hewa.
Africa Newss
CHANZO: MWANANCHI
Chapisha Maoni