0
KATIKA kuhakikisha vijana nchini wanajiajiri, Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) na Benki ya TIB, wameingia mkataba wa kuwawezesha kwa mikopo wajasiriamali vijana wanaomaliza vyuo vikuu nchini na vingine vya kati ili waweze kujiajiri.

Katika makubaliano hayo, TIB itatoa mikopo hiyo na kwa kuanzia kiasi cha Sh bilioni 1 kimetengwa kwa ajili ya mpango huo utakaoratibiwa na NEEC,
ambayo itakuwa na jukumu la kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana hao, ikiwa ni pamoja na kusaidia namna ya kutayarisha andiko la miradi kwa nia ya kuomba mikopo.

Katika makubaliano hayo yenye lengo la kusaidia vijana kujikita katika miradi ya kilimo, uzalishaji, biashara na huduma, viwango vya mikopo vitakavyotolewa ni Sh zisizozidi milioni 200 kwa vikundi, washirika au ushirika, wakati kwa
mjasiriamali mhitimu wa chuo kikuu,
atakopesheka hadi Sh milioni 50.

Hata hivyo, watakaokopesheka ni wale
watakaofaulu mafunzo ya kuwaandaa
wajasiriamali, yatakayokuwa yakitolewa na NEEC.
Waliosaini mkataba huo ni Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Peter Noni na Katibu Mtendaji wa NEEC, Dk Anacleth Kashuliza katika ofisi za benki
hiyo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo, Dk Kashuliza alisema vijana wengi wanamaliza vyuo vikuu, lakini wanakosa cha kufanya kutokana na tatizo kubwa la ajira.

Alisema Benki ya TIB na NEEC wamekubaliana kuanzisha mfuko wa kuwakopesha vijana, watakaoandika michanganuo ya miradi ambayo
itakidhi vigezo vya kukopeshwa.
Alisema vijana wengi wanakabiliwa na
changamoto ya kuandika miradi bora hivyo kupitia mradi huo ambao ni endelevu, watawapa elimu ya ujasiriamali pamoja na ujuzi wa kuandika michanganuo.

Kwa upande wake, Noni alisema vijana wengi wanakabiliwa na changamoto ya kupata dhamana kwa ajili ya mikopo, hivyo mfuko huo unaweza
kuwa mkombozi kwao.
“Vijana watapata mikopo ya mitaji isiyohitaji dhamana ambayo watatakiwa kuirejesha ndani ya miaka mitatu, hivyo tunawahamasisha vijana wanaomaliza vyuo vikuu wachangamkie fursa
hii,” alisema Noni.

Alisema vijana watakaokopeshwa, watakuwa kwenye vikundi vikundi na hata mmoja mmoja, kwani watakachoangalia si ukubwa au wingi wa watu, bali ni ubora wa mradi ulioombewa mkopo.

Chapisha Maoni

 
Top