0
Kundi la watu wanaodhaniwa ni majambazi, wamevamia na kupora fedha taslimu na vitu mbalimbali katika Kanisa Katoliki la Kilema, Jimbo
la Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Desemba 14, mwaka huu, ambapo watu hao wakiwa na vifaa maalumu vya kuvunja milango, walivunja lango
kuu la kanisa hilo, kuvunja sanduku la sadaka na kupora vifaa vya kufanyia ibada.

Kanisa hilo ni la kwanza kujengwa na Wamisionari wa kwanza Kanda ya Kaskazini, inayojumuisha mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Dodoma.
Akizungumza kwa njia ya simu jana, Padri wa Parokia ya Kilema, Damien Temere Mosha, alisema vitu vilivyoibwa ni pamoja na vifaa vitakatifu vinavyotumika katika sikukuu ya Ekaristi.

Akizungumza na mwandishi, Paroko wa Parokia ya Kilema, Padri Mosha alisema majambazi hao walivunja kasha la kuhifadhi sadaka na kupora fedha zilizokuwamo, ambazo hazijajulikana
thamani yake.

Alisema majambazi hao waliiba vifaa vya kunywea divai na komunio, ambavyo ni vya dhahabu. Padri Mosha alisema majambazi hao walivunja kasha
maalumu la kuhifadhi vifaa vya ibada na kuiba vile vya dhahabu tu vyenye thamani ya mamilioni ya fedha huku wakiacha vya shaba.

Alisema baadhi ya vifaa hivyo vilinunuliwa na wamisionari wa kwanza na vilikuwa na thamani kubwa kwa Kanisa hilo, kwa kuwa viliwakilisha
imani katika parokia hiyo na Kanda nzima ya Kaskazini.

Kiongozi huyo wa kanisa alibainisha kuwa jambo lililomsikitisha ni namna eneo takatifu la kanisa hilo lilivyoharibiwa vibaya, kwani eneo hilo mara nyingi limekuwa likitumika kwa ajili ya kutolea sakramenti takatifu kwa mujibu wa utamaduni wa
Kanisa hilo Katoliki.

Aliwataka wakazi wa Kilema na wanaozunguka eneo hilo kuwa na utulivu wakati huu vyombo vya
usalama vikiendelea na uchunguzi hadi pale waliohusika na tukio hilo watakapokamatwa na kuchukuliwa hatua.

Waumini wa kanisa hilo ambao walikusanyika kwa ajili ya sala yao ya kawaida ya Jumapili majira ya
saa moja asubuhi, walijikuta wakichelewa kuanza misa wakati uongozi wa kanisa hilo, ukijaribu
kutengeneza na kusafisha maeneo yote
yaliyoharibiwa na majambazi hao.

Nje ya mlango wa kuingilia kutoa sadaka, kulikuwa na damu na inasadikiwa kuwa huenda ni za mmoja wa watu hao waliovamia kanisa hilo
alijeruhiwa wakati akijaribu kuvunja mlango huo, ambao hufungwa kwa vitasa imara.

Mosha alisema katika tukio hilo, hakuna mtu aliyejeruhiwa au kupoteza maisha. Paroko huyo alitangaza kuwa kanisa litatoa zawadi ya Sh milioni mbili kwa mwananchi yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwa majambazi hao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Geofrey Kamwela alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Alisema taarifa rasmi itatolewa baada ya
uchunguzi kukamilika.

Chapisha Maoni

 
Top