Mtoto mmoja mwenye umri wa mwaka mmoja amefariki dunia baada ya kunywa pombe ya kienyeji aina ya Mtukulu inayosadikiwa kuwa na
sumu mkoani Singida.
Kamanda wa Polisi Mkoani Singida ACP Thobias Sedoyeka amethibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea majira ya saa 3 asubuhi siku ya Alhamisi tarehe 08 Januari, 2015 na kusema kuwa
mama wa mtoto amelazwa katika hospitali ya Makingu kwa matibabu.
Akielezea mazingira ya tukio hilo, Kamanda Sedoyeka amesema mama wa mtoto huyo akiwa na mwanaye, alihudhuria sherehe iliyokuwa imeandaliwa na jirani yake maalum kwa ajili ya kusherehekea kuanza kwa msimu wa kilimo kutokana na mvua kuanza kunyesha.
Baada ya kufika katika sherehe hiyo iliyokuwa imehudhuriwa pia na majirani wengine, ndipo walipoanza kunywa pombe hiyo, ambapo mama
huyo anadaiwa kumywesha pia mwanaye huyo na muda mfupi baada ya kunywa wote (mama na
mtoto) walianza kutapika na kuharisha.
Baada ya hali kuwa mbaya, walikimbizwa hospitali ambapo mauti yalimkuta mtoto huyo, na mama mwenyewe bado anapatiwa matibabu.
Chapisha Maoni