ZAIDI ya walimu 200 wa shule za msingi na sekondari za Manispaa za Kinondoni, Dar es Salaam jana wameandamana hadi katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo wakitaka kutekelezewa madai mbalimbali wanayoidai
manispaa hiyo, zikiwamo fedha za likizo pamoja na kupandishwa madaraja.
Walimu hao wa shule za msingi na sekondari walinza kuandamana saa 5.00 asubuhi katika Ofisi za Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya
Kinondoni walipokwenda kuhoji juhudi za chama
hicho katika kushughulikia matatizo yao.
Baada ya kufika katika ofisi hizo, walimu hao walianza kutoa shutuma kwa uongozi kwa kutoshughulikia madai yao kikamilifu na hivyo kuwafanya waendelee kuteseka, hatua iliyowafanya
kuwalazimisha viongozi hao kuongozana nao hadi kwa Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Mussa Natty.
Huku wakiimba nyimbo mbalimbali za
mshikamano ukiwamo wa ‘Solidarity
Forever’ (Mshikamano daima), walimu hao na viongozi wa CWT walikwenda kwenye ofisi ya Manispaa ya Kinondoni kwa lengo la kuonana na mkurugenzi lakini walizuiliwa getini.
Hata hivyo, pamoja na kuzuiliwa na askari wa Manispaa ya Kinondoni kuingia ndani ya ofisi za manispaa hiyo, walipenya kwa kutumia njia
mbalimbali zinazozunguka ofisi hizo na kuwaacha walinzi wakishindwa la kufanya.
Aidha, walipoingia ndani ya ofisi hizo, walimu hao waliendelea kuimba nyimbo mbalimbali huku wakimtaka Mkurugenzi kujitokeza na kuzungumza nao ili ajue hatma yao huku wakisisitiza
kutoondoka eneo hilo kama kiongozi huyo asingejitokeza.
Hali hiyo ilifanya baadhi ya wafanyakazi wasitishe kazi kwa muda na kuchungulia madirishani na wananchi waliokwenda kupata huduma wakapatwa na mshangao wa kilichokuwa kikiendelea.
Baada ya dakika 20 tangu walimu hao kuwasili mahali hapo, Mkurugenzi huyo alijitokeza na kuzungumza nao na kuahidi kulishughulikia suala hilo haraka iwezekanavyo na kuwataka kusubiri
majibu yao ndani ya kipindi cha mwezi mmoja kuanzia jana.
Baada ya majibu hayo, walimu hao wakiongozwa na viongozi wa CWT waliondoka eneo hilo na kuongozana hadi ofisi za chama hicho kwa kikao
cha muda mfupi kilichotoa uamuzi wa walimu hao kuendelea na majukumu yao kusubiri utekelezaji ulioahidiwa na Mkurugenzi wa Kinondoni wa
kushughulikia madai yao.
Mwalimu mwingine Huruma Minga, alisema madai ya walimu hao katika manispaa hiyo ni mengi na mengine yanakatisha tamaa huku akishangazwa
na utaratibu wa upandishwaji wa madaraja unavyofanyika kwa madai kuwa kuna upendeleo.
“Kuna wakati mtu unajaza fomu ya likizo na pengine kwa utaratibu wako unatakiwa ulipwe fedha kiasi cha Sh 400,000 lakini unaweza kujikuta ukilipwa Sh 60,000 na wakati huo hata ile
fomu ya likizo ulioijaza hujajua mahali
ilipopelekwa, hivyo kujikuta unapoteza haki yako,” alisema Huruma.
Mbali na hilo alisema utaratibu wa kuwapandisha madaraja walimu katika manispaa hiyo una mianya ya upendeleo kwa baadhi ya walimu na kwamba hadi sasa wapo baadhi hawajapanda hata
daraja moja katika kipindi cha zaidi ya miaka kumi ya ufundishaji.
Alisema lakini wapo wengine ambao kila baada ya miaka miwili wanapanda madaraja huku, akidai kushangazwa na walimu waliopo masomoni kutopewa barua za kupanda madaraja hayo.
Akizungumzia maandamano hayo, Katibu wa CWT wilaya ya Kinondoni Stephen Mnguto, alisema hatua hiyo imetokana na walimu hao kuchoshwa
na ‘ubabaishaji’ wa viongozi wa manispaa hiyo jambo ambalo hata wao liliwafanya wasiaminike
mbele ya wanachama wao.
Alisema kimsingi madai ya walimu hao
yangeweza kuwa yamemalizwa kwa kuwa mengi yana muda mrefu hivyo hakukuwa na haja kulimbikizwa hadi muda huu wakati suala hilo lipo
wazi.
“Yapo madai ya walimu kutopandishwa madaraja kwa wakati, katika kipindi cha mwaka 2013/ 14 zaidi ya walimu 1,743 walitakiwa kuwa wamepandishwa madaraja lakini hadi leo hakuna
lililotekelezwa,” alisema Mnguto.
Alisema licha ya madai hayo yapo madai ya baadhi ya walimu waliopo masomoni kutopewa barua hizo achilia mbali fedha za likizo alizodai kuwa hazijatolewa kwa walimu zaidi ya 300.
Hata hivyo, kupitia katibu huyo, walimu hao walisema wanasubiri utekelezaji huo huku wakisubiri kujua hatua zipi wazichukue endapo suala hilo halitotekelezwa kama walivyoambiwa.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba katika taarifa yake aliyoitoa bungeni Novemba mwaka jana, walimu nchini walikuwa wakiidai serikali jumla ya Sh bilioni nne.
Chapisha Maoni