Evangelical Assemblies Of God –Tanzania (IEAGT)
lililopo katika kata ya Kambarage katika manispaa
ya Shinyanga ambapo leo Jumapili Juni 26,2016
kumefanyika Maombi Maalumu kwa ajili ya taifa la
Tanzania, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt John Pombe Magufuli,makamu wa
rais,bunge,mahakama,polisi na viongozi
mbalimbali wa serikali.
Maombi hayo yameongozwa na askofu wa kanisla
la (IEAGT) David Elias Mabushi na kuhudhuriwa
na kaimu mkuu wa mkoa wa Shinyanga
Mheshimiwa Josephine Matiro ambaye ni mkuu
wa wilaya ya Shinyanga.
Maombi hayo pia yamehudhuriwa na viongozi
mbalimbali wa serikali,vyama vya
siasa,mashirika,waandishi wa habari,wageni
mbalimbali na waumini wa kanisa hilo.
Pamoja na maombi hayo maalumu, Kanisa hilo
limeadhimisha siku ya watoto katika kanisa hilo
ambapo pia Juni 26 ni siku ya kuzaliwa kwa
askofu wa kanisa la IEAGT David Mabushi ambaye
leo ametimiza umri wa miaka 53.
Sambamba na matukio hayo mawili
makubwa,kanisa hilo pia lilikabidhi madawati 20
kwa uongozi wa wilaya ya Shinyanga kwa ajili ya
kumuunga mkono rais Magufuli katika jitihada
zake za kuhakikisha kuwa changamoto ya
madawati inamalizika katika shule.
Awali akisoma risala,Katibu wa kanisa la IEAGT,
Mchungaji Obed Jilala alisema baada ya uchaguzi
mkuu 2015,kanisa la IEAGT limekuwa likisikia kwa
nyakati tofauti rais Magufuli akiomba maombi kwa
ajili ya kazi yake ya kuliongoza taifa,hivyo kanisa
lao limeguswa sana na kauli hiyo na katika
kuonesha wanamuunga mkono walikubaliana siku
ya Jumapili Juni 26,2016 iwe ya maombi
maalumu kwa ajili ya kiongozi wa taifa sambamba
na kuliombea nchi ya Tanzania.
"Maombi haya yamebebwa kwa kiasi kikubwa na
upendo tulio nao kwa nchi yetu ,kanisa la IEAGT
kama sehemu ya jamii ya watanzania tumeona
siku ya leo iwe kilele cha maombi ya kitaifa
katika mkoa wetu na mahali popote lilipo kanisa
letu",aliongeza Mchungaji Jilala.
Naye Askofu wa kanisa hilo David Mabushi akitoa
mahubiri yake,mbali na kumpongeza rais Magufuli
kwa kuchaguliwa kuwa rais,alimuomba kuendelea
kuonesha msimamo wake katika kuwaletea
maendeleo watanzania huku akimfananisha na
Nabii Musa akisema Magufuli amekuja
kuiokomboa nchi na kuifanya kuwa nchi ya asali
na maziwa.
"Tumeandaa siku hii muhimu kwa ajili ya
kuiombea nchi yetu ili iendelee kuwa na
amani,tunamuombea rais wetu kwa sababu wenye
haki wakiwa na amri,watu hufurahi..sisi kama
kanisa tutahakikisha tunamuunga mkono rais
Magufuli kwa maneno na vitendo ndiyo maana leo
tunatoa sadaka ya madawati 20,tunaomba
watanzani waendelee kumuombea rais wetu
aliyeonesha kuwajali watanzania tangu alipoingia
madarakani amekuwa mstari wa mbele kupigana
dhidi ya rushwa na vitendo vyote viovu",aliongeza
askofu Mabushi.
Kwa upande wake mgeni rasmi Kaimu Mkuu wa
mkoa wa Shinyanga ,Josephine Matiro ambaye ni
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine
Matiro,alilipongeza kanisa hilo kuona umuhimu wa
kuombea viongozi wa nchi na kuongeza kuwa
kanisa la IEAGT ni kanisa la kwanza mkoani
Shinyanga kufanya maombi kwa ajili ya viongozi
wa nchi.
"Ndugu zangu watanzania naomba tuendelee
kuiombea nchi ili iendelee kuwa ya amani na
viongozi kuwa na hofu ya mungu,lakini pia
naomba watanzania wafanye kazi,sasa ni muda
wa kuchapa kazi tuache siasa za
majukwaani,tumuunge mkono mheshimiwa rais
katika kutekeleza kauli mbiu ya Hapa Kazi
tu",aliongeza Matiro.
Miongoni mwa mambo yaliyoombewa katika ibada
hiyo ni kuombea taifa,kumuombea rais
Magufuli,makamu wa rais,waziri mkuu na viongozi
wengine wa serikali,kuombea bunge na
madiwani,kuombea mahakama na katika maeneo
yote viongozi wa dini waliwataka viongozi hao
kuwa hofu ya mungu na kuchukia rushwa pamoja
na kutumia nguvu zao kupambana na vitendo vya
kihalifu ikiwemo mauaji ya watu kwenye nyumba
za ibada,vikongwe,albino na watu mbalimbali
wasio na hatia.
Chapisha Maoni