0

MSAJILI wa Vyama vya Siasa Nchini, Jaji
Francis Mutungi ametetea kauli ya Rais John
Magufuli kuhusu kufanya siasa wakati huu na
kwamba alichotaka kiongozi huyo wa nchi ni
ushirikiano kutoka kwa wanasiasa wenzake ili
kuwaletea maendeleo wananchi.
Alisema Rais Magufuli, katika kauli yake ile
hakumaanisha kuzuia shughuli za siasa nchini
isipokuwa alieleza kuwa hatakuwa tayari
kuona siasa zinakwamisha mikakati ya
kuwapelekea wananchi maendeleo yao.
Jaji Mutungi alisema hayo Dar es Salaam jana,
alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu kauli ya
Rais Magufuli ya kuwataka watu kuacha siasa
za hovyo hadi mwaka 2020 utakapofanyika
uchaguzi mkuu mwingine, ili muda uliopo
wautumie kuijenga nchi.
Alisema siyo kwamba Rais anapinga siasa
isipokuwa anapingana na wanasiasa ambao ni
pingamizi katika kuleta maendeleo na muda
wote wamejikita katika siasa bila kuangalia
namna ya kutekeleza ahadi zao kwa wananchi.
Alisema wapo watu walioitafsiri tofauti hotuba
aliyoitoa juzi Rais Magufuli, hivyo wananchi
wanapaswa kuwa watafiti na kuweka maslahi
ya nchi huku akiwataka wanasiasa kuwa
wavumilivu na kutumia muda wao kutafakari
jambo kabla ya kuzungumza.
Alisema dhamira ya Rais ni kuwaletea
maendeleo kwa wananchi na taifa kwa ujumla
na vyama vinapaswa kufuata utaratibu wa
kuwasilisha taarifa kwa msajili na si kusubiri
hadi vyombo vya habari kutoa taarifa.
Mutungi alisema vyama vya siasa vimekuwa
vikitaka demokrasia nchini, hivyo kabla ya
vyama kufikiria demokrasia kitaifa, hivyo
viongozi wake waanze kuangalia suala hilo
kwenye vyama vyao na si kuimba, kwani wapo
wanaofanya ndivyo sivyo.
Alisema mtu anapotetea jambo, kwanza
anapaswa kulitekeleza kwa vitendo huku
akibainisha demokrasia kutotokea nchini
endapo demokrasia ndani ya vyama vya siasa
kuwa ni shida.
Jaji huyo alisema bado kuna kazi kubwa huku
akibainisha yapo mambo mengi yanayotokea
nchini huku akitegemea ushirikiano wao na
kuwataka wanasiasa kuwekeza katika kufanya
upembuzi wa mambo kabla ya kutamka au
kuyatenda.
Naye Msajili Msaidizi, Kitengo cha gharama za
Uchaguzi na Elimu kwa Umma, Piencia Kiure
alisema ni vyama vitatu tu kati ya 22 ndivyo
vimewasilisha taarifa ya gharama za Uchaguzi
Mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana.
Mwisho wa kuwasilisha gharama hizo ni leo.
Alivitaja vyama vilivyowasilisha gharama za
uchaguzi kuwa ni Chama Cha Mapinduzi
(CCM), ACT-Wazalendo na Chama cha
Wananchi (CUF).
Alifafanua kuwa, mgombea atakayeshindwa
kuwasilisha gharama za uchaguzi
utahukumiwa kifungo kisichozidi mwaka
mmoja au faini isiyozidi Sh milioni mbili au
vyote kwa pamoja.
Aidha, chama kitakachoshindwa kuwasilisha
gharama za uchaguzi katika kipindi
kilichowekwa adhabu yake ni faini isiyozidi Sh
milioni tatu na kutoruhusiwa kushiriki
uchaguzi hadi watakapofanya marejesho.

Chapisha Maoni

 
Top