Tumepokea kwa mshtuko mkubwa kauli na
maagizo ya Rais kuhusiana na haki ya kufanya
shughuli za kisiasa ikiwemo mikutano ya hadhara,
makongamano na hata maandamano kwa vyama
vya siasa.
Tumetafakari kwa kina kama kweli Rais anafahamu
vyema sheria zinazotawala na kuongoza siasa
katika nchi anayoiongoza.
Aidha, tumejiuliza sana kama Rais wetu na
washauri wake... kama anao na kama
anawatumia.... wanamsaidiaje Rais ili kumwepusha
na kauli tata za mara kwa mara ambazo huzua
taharuki na ukakasi usio wa lazima.
Wakati bado tunaendelea kudadisi maana ya
demokrasia na tafsisri ya nini ni siasa kwa uelewa
wa Rais wetu tunapenda kusema yafuatayo:
1. Rais anastahili kujua kuwa siasa siyo starehe
bali ni kazi kama zilivyo nyingine zozote.
2. Siasa siyo tukio la uchaguzi bali ni maisha yetu
ya kila siku. Ni mfumo unaogusa maisha yetu ya
kila siku! Ni lifestyle.
3. Uhalali wa kazi za siasa unatolewa na Katiba
aliyoapa kuilinda na kukaziwa na sheria namba 5
ya mwaka 1992 (Political Parties Act NO. 5 of
1992) pamoja na marekebisho yake.
Uhalali huo ndiyo unaomfanya yeye kuwa Rais leo
na ndiyo unaotoa uhalali wa chama chake kuwepo
na kutekeleza kihalali na kisheria majukumu yake
ya kila siku.
4. Sheria hizi zimenyumbuisha uwepo wa Ofisi ya
Msajili wa vyama vya siasa na majukumu ya
vyama vya siasa kama yanavyotambuliwa na
katiba za vyama husika na maagizo ya Rais
hayawezi kuwa mwongozo wa lini na namna
vyama vinavyopaswa kujiendesha.
Uhalali na haki ya kazi za Siasa hazitolewi na
“mapenzi” ya Rais bali na Katiba na Sheria za
nchi.
5. Haki ya kufanya siasa haiwezi kuwa miliki ya
Serikali, Wabunge na Madiwani pekee kama
anavyoagiza Rais!!
Akumbuke uchaguzi mkuu siyo tukio pekee la
kisiasa. Kuna chaguzi za serikali za mitaa, chaguzi
za marudio na mambo mengine mengi.
Ni wajibu wa msingi wa vyama vya siasa kufuatilia
utendaji kazi wa kila siku kwa wale wanaoongoza
Serikali na hivyo siasa siyo uchaguzi pekee.
6. Elimu ya Uraia na elimu ya siasa ni wajibu
mkuu wa vyama vya siasa nayo hustahili kutolewa
wakati wote na siyo na wanasiasa wa kuchaguliwa
au kuteuliwa pekee!!
7. Rais anapaswa kutambua kuwa hata yeye
anatokana na chama cha siasa. Anapaswa kubaini
kuwa vyama vya siasa vina miundo ya viongozi na
watendaji nchi nzima ambao majukumu yao ni ya
muda wote na siyo ya msimu wa uchaguzi pekee.
8. Rais anapaswa kuelewa kuwa mwisho wa
uchaguzi mmoja ni mwanzo wa uchaguzi
mwingine.
9. Makongamano yakiwemo ya siasa
anayolalamikia Rais ni pamoja na Kigoda cha
Mwalimu J.K. Nyerere ambalo lilionekana kuhoji
mambo kadhaa yanayogusa mustakabali wetu
kama nchi!!
Makongamano katika vyuo na taasisi mbalimbali ni
sehemu muhimu ya taaluma na huibua uelewa
muhimu kwa jamii.
10. Makongamano mengi huandaliwa na taasisi
zisizo za kiserikali na taasisi za dini. Raisi
anastahili kutambua kuwa siasa inamgusa kila
mmoja kwani siasa ni maisha ya watu.
11. Walianza kwa kulithibiti Bunge na Wabunge wa
Upinzani kwa kujaza askari bungeni kama vile ni
uwanja wa vita;
Wakathibiti haki ya msingi ya wananchi kufuatilia
mijadala ya Bunge kupitia matangazo ya “live”
kisha “kuondoa” kimkakati uhuru wa vyombo vya
habari katika kuhoji na kuchambua kwa uhuru
habari mbalimbali “zisizowapendeza” watawala
sambamba na utekelezaji wa sheria
inayolalamikiwa sana ya “Cybercrime”!
Ikafuata Uchakachuzi wa Uchaguzi wa Rais wa
Zanzibar na Baraza la Wawakilishi; Wakaendelea
kwa kutimua timua wabunge wa vyama vya
upinzani Bungeni;
Leo ni vyama vya siasa vya Upinzani kupewa
“likizo ya lazima ya Rais”; kesho inaweza ikawa
taasisi za dini, baadaye asasi zisizokuwa za
kiserikali na hatimaye nchi hii itaweza kugeuka
nchi ya utawala wa mabavu ya kutumia dola
(Authoritarian Regime).
12. UKAWA hatutakubaliana na hali hii. Hili ni
tamko la hatari kwa Demokrasia, Utawala wa
sheria, haki za binadamu na linakinzana na kila
aina ya Uhuru ambao katiba yetu aliyoapa kuilinda
Rais, imetoa.
13. Kwa uzito wa kauli hii vyama vyetu vitafanya
vikao vyake haraka iwezekanavyo na kutoa kauli
rasmi.
14. Tunawasihi Watanzania wote wakatae na
wapuuze utamaduni huu mpya unaoonekana
kutengeneza utawala wa kidikteta na ambao ni
dhahiri utabomoa mshikamano wetu kama Taifa.
15. Rais kuwa mkali katika kusimamia uwajibikaji
na utendaji wa Serikali ni jambo jema lakini
linapoteza maana kama ukali huo unatumika
kuvunja Katiba na Sheria sambamba na kuziba
watu midomo. “Freedom” ni jambo la kupigania na
kutetea kwa gharama yoyote ile na tuko tayari kwa
wajibu huo.
16. Wanaoweza kumshauri Rais na wafanye hivyo
kwani athari za jambo hili ikiachiwa ikaota mizizi
hata hayo maendeleo anayoyapigania Rais
yanaweza kubaki kuwa ndoto na nchi kuingizwa
kwenye machafuko yasiyo ya lazima.
Freeman Mbowe,
Mbunge wa Hai,
Mwenyekiti CHADEMA Taifa
Na Kiongozi wa upinzani Bungeni.
Chapisha Maoni