0
Mwenyekiti wa zamani wa Klabu ya Simba Ismail
Rage, amewataka viongozi waliopo madarakani
kupunguza malumbano na wachezaji ili kujenga
kikosi imara ambacho kitarudisha heshima ya timu
hiyo kwa kufanya vizuri katika mashindano
mbalimbali watakayoshiriki yakiwemo yale ya
kimataifa.
Rage alisema kufanya vibaya kwa timu hiyo
kumetokana na viongozi kuwafukuza wachezaji
wazuri bila sababu za msingi jambo ambalo
limechangia timu hiyo kushindwa kufanya vizuri
kwa sababu kila msimu timu hiyo inakuwa na
idadi kubwa ya wachezaji wapya.
“Niseme ukweli kwamba Yanga ndiyo timu bora
hivi sasa hapa kwetu Tanzania kwa sababu
wamesajili wachezaji wazuri wenye uwezo na
wamekaa pamoja kwa muda mrefu tofauti na
Simba yetu ambayo kila msimu tunakuwa tukisajili
wachezaji wapya ambao wamekuwa wakihitaji
muda kuzoeana na wengine wamekuwa
wakifukuzwa pasipo sababu za msingi,” alisema
Rage.
Kiongozi huyo alisema kitu kingine ambacho
kimekuwa kikwazo cha mafanikio ya Simba ni
uongozi kuogopa vikao vya wanachama ambavyo
kwa asilimia kubwa vinakuwa na nia njema ya
watu hao kutaka kujua mwenendo wa timu yao na
kuwaweka wazi namna ya uendeshwaji wa klabu
yao.
Alisema wakati wa uongozi wake aliwahi
kukumbana na jambo hilo mara mbili, lakini
alijitahidi kuhakikisha wanachama wanapata haki
yao ya msingi na kikatiba kwa kukutana nao na
kusikiliza mawazo yao na aliyafanyia kazi ingawa
hawakuweza kufanya vizuri katika msimu wake wa
mwisho.
“Mimi nawashauri wenzangu kutanguliza busara
mbele na wasiogope vikao vya wanachama pia
nawatakia mafanikio mema kuelekea Mkutano
Mkuu utakaofanyika Julai 10, mwaka huu cha
msingi wajitahidi kufanya usajili mzuri msimu huu
kwa kutumia pesa za usajili wa Emmanuel Okwi na
Mbwana Samatta, ili kurudisha mafanikio ya
Simba,” alisema.
Mara ya mwisho Simba kutwaa ubingwa wa Ligi
Kuu ya Tanzania Bara, ilikuwa msimu wa 2011/12,
ikiwa chini ya uongozi wa Rage tangu hapo timu
hiyo imekuwa ikipambana kurudia mafanikio hayo
licha ya kubadilisha uongozi kuingia Evans Aveva,
lakini imekuwa ikiishia kumaliza katika nafasi ya
tatu na nne.

Chapisha Maoni

 
Top