katika utendaji kazi wao bila kusubiri majambazi
kufikia hatua ya kuwanyang’anya silaha katika
vituo au kuvamia nyumba, watu na
kuwanyang’anya mali zao.
Aidha, alisema umefikia wakati wa polisi sasa
kugangamala na kutosita kuwanyang’anya
majambazi silaha haraka na akiwataka kutumia
mbinu za medani kwani wananchi wamechoka
kutafuta mali zao huku watu wengine wakija
kuchukua na kuahidi kuangalia namna ya
kuwanunulia helikopta kwa ajili ya doria.
Magufuli alisema hayo jana jijini Dar es Salaam
wakati akizindua mpango wa usalama wa raia
katika kuboresha utendaji kazi kwa kutumia Mfumo
wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) awamu ya pili
unaoanza kutekelezwa katika wilaya ya Kinondoni
Julai mosi mwaka huu na baadaye kusambaa nchi
nzima baada ya miaka mitatu na kupunguza
uhalifu kwa asilimia 10 kila mwaka.
Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na Rais mstaafu wa
Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na Katibu Mkuu
Kiongozi John Kijazi. “Naomba niwe mkweli na
muwazi kwa sababu sitaki kuwa mnafiki kwani
yapo mambo yalikuwa yakinikereketa na kuniudhi
unapoona jambazi anavamia kituo cha Polisi na
kuua polisi kisha kuondoka na silaha au
anakwenda kuiba mahali na ana silaha anaondoka
hivi hivi hili limekuwa linanipa wasiwasi kidogo.
“Kama mnazo bunduki za kutosha kwa nini
jambazi aondoke bila kunyang’aywa silaha
anayotumia haraka haraka ,ninaposema haraka
haraka mnanielewa, kwa nini jambazi aende mahali
akafanye ujambazi na polisi mshindwe
kumnyang’anya silaha yake haraka haraka,” alihoji.
Alisema polisi wanazo bunduki na risasi suala ni
kumnyang’anya jambazi bunduki yake haraka kwa
sababu kama ameenda mahali na bunduki
hakwenda kwa ajili ya maonesho na kutoa wito
kwa polisi nchini wakimuona jambazi ana silaha
wahakikishe wanamnyang’anya bunduki yake
haraka.
Rais Magufuli alisema na yule polisi atakayekuwa
amejitoa mhanga kumnyang’anya bunduki jambazi
asipelekwe mahakamani ila apewe cheo kwani
hakuna polisi jamii kati ya jambazi na polisi.
“Nasema kwa dhati kuwa mna mbinu nyingi za
kuwanyang’anya silaha majambazi ,kwani wakati
mwingine unaweza kumuita tu na akakubabidhi
silaha ni vyema kutumia hizo mbinu na nyingine
mnazoziita za medani MM na mkifanya hivi IGP
mtanifurahisha,” alisema.
Magufuli alisema wananchi wamechoka kwani
wanapata mali zao kwa kuhangaika lakini anakuja
jambazi kuchukua na kutoa mfano jijini Dar es
Salaam ambapo wanawake wamekuwa waathirika
wa matukio ya kuporwa.
“ Unakuta mwanamke anatembea na pochi au
simu anakuja mtu na bodaboda na kumburuta na
kuchukua mkoba wake na polisi mpo”. Aliwahoji
kwa nini polisi wasijifanye kuchukua ‘boda’ na
kuwashika haraka haraka watu wanaofanya vitendo
hivyo kwani wakiamua Tanzania iwe na amani
itakuwa na amani.
Alitoa wito kwa wakubwa wa Jeshi la Polisi ambao
ni IGP na makamanda wake kuwa vijana wao
wanaweza kuwa na moyo wa kufanya kazi lakini
wanawabana na kuwachelewesha kufanya kazi
kwani wakienda kusaka majambazi polisi hupewa
maelekezo wasiwanyang’anye silaha.
Alisema wao wanakuwa kwenye vituo vya mbali
hivyo siku nyingine atawapeleka wakubwa hao wa
Jeshi la Polisi watangulie kuwanyang’anya
majambazi silaha. Rais Magufuli alisema jeshi hilo
lina vijana wazuri na imara wanaopenda kazi zao
na yeye kusisitiza kuwa ataendelea kusimamia
maslahi ya polisi kwani tatizo ni uwezo lakini kadri
wanavyoenda mambo yatakuwa mazuri.
“Ni vyema mtusaidie nchi iwe kama nyingine hata
ukisahau pochi yako unaikuta kama nchi jirani ya
Rwanda ukisahau hata pochi yako unaikuta hata
kesho kwa nini hapa isiwe, polisi mkiamua
mnaweza,” alisema.
Alieleza kuwa kwa mfumo huo ambao wameweka
wa kufuatilia kila kitu wataangalia kwa upande wa
serikali kama kuna mabaki watawaongezea lakini
yatumike kama yalivyokusudiwa kwani nao polisi
wanalalamikiwa kutumia fedha vibaya.
Alisema suala hilo nalo linatia dosari lakini
yaliyopita basi yaangaliwe yaliyopo na yajayo kwa
kwenda vizuri ili nchi iwe na amani kwani
Watanzania wana imani na Jeshi la Polisi. Rais
alisema asilimia kubwa ya maaskari ni wazuri
lakini wale wachache wasio waaminifu ni vyema
wakatolewa kwani licha ya mpango huo kuwa
mzuri mtu anaweza kupiga simu kisha jambazi
akaambiwa na mtoa taarifa akashughulikiwa au
taarifa za wasamaria zikasambaa suala ambalo lipo
Polisi.
Alieleza kuwa wale vijana wanaokadiriwa 100
watakaofanya kazi kwa awamu ambao watakuwa
wakipokea simu na taarifa za uhalifu utakaokuwa
ukiendelea ni lazima wapewe posho maalumu na
lazima wawe vijana wenye maadili kwa
kuwachunguza pamoja na uangalizi maalumu.
Alitoa wito pia kwa wananchi wote kuendelea
kuliamini Jeshi la Polisi na kushirikiana nalo huku
wakitoa taarifa ili nchi iendelee kuwa salama kwani
kwa ushirikiano wao ana uhakika wataweza
kushinda masuala ya ujambazi na uhalifu
unaotokea.
Rais Magufuli alisema hakuna sababu ya Dar es
Salaam maduka kutofunguliwa usiku au kufanya
biashara usiku lakini inawezekana wafanyabiashara
wanahofia usalama wao hivyo mazingira yajengwe
kuhakikisha kunakuwa na amani. Huku akitaka
katika miji yote kufungwa kamera za CCTV kwani
siyo vigumu wala vya gharama na vikiunganishwa
katika mpango huo uhalifu utamalizika kwa haraka
zaidi.
Alisema Kinondoni inasifika kwa matukio mengi ya
uhalifu ambapo mwaka 2012 kulikuwa na matukio
ya uhalifu 4,410 lakini mpaka kufikia mwaka 2015
vitendo vya uhalifu vilifikia 8,804.
Aliomba mpango huo uliozinduliwa Kinondoni kwa
mwaka huu na miaka ijayo uhalifu ushuke na
ndiyo itakuwa matokeo mazuri ya mpango huo
lakini uhalifu ukipanda kutakuwa hakuna sababu
ya kuwa na mpango huo.
Rais pia alimuagiza Katibu Mkuu Kiongozi
kuwaagiza Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) ambao
wana wajibu wa kushirikiana na polisi kwa mtu
anapopiga simu katika namba 111 au 112 kusiwe
na mtu wa chapa bali inapopigwa inakiliwe na
kuchapwa moja kwa moja.
Alisema vyote ni vyombo vya serikali hakuna
sababu ya TCRA kutofanya hiyo kazi na asiyetaka
kufanya hivyo aondoke kwani atakuwa hataki
kushirikiana na polisi kudhibiti uhalifu.
Kuhusu wanasiasa Alisema atafanya kazi bila
kuwabagua watu kwa vyama vyao, maeneo
wanayotoka makabila, dini kwani yeye kwake ni
kazi tu kwani Watanzania wanahitaji maendeleo na
vyama kuweka pembeni kwani wanataka kero zao
kumalizwa na kuishi maisha mazuri.
Rais alisema yapo aliyoahidi kutekeleza kwa miaka
mitano hivyo wamuache atekeleze kwa ajili ya
Watanzania wote wakiwemo viongozi wengine wa
vyama kama Diwani wa eneo hilo wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamuache
atekeleze na CCM wasimsumbue kwani
watamuuliza baada ya miaka mitano.
Alisema aliyoyaahidi hategemei mtu mmoja
kumchelewesha kutekeleza hayo, kwani anataka
baada ya miaka mitano kupimwa kwa aliyoyaahidi
kwa hiyo polisi wasimamie watu
wasiwacheleweshe kutekeleza aliyoyaahidi. “Najua
mmenielewa ‘Message sent and Delivery’ kwani
ndugu zangu hamtaki nitekeleze yale niliyoahidi?”
Alijibiwa na umati wa watu kuwa wanataka. Naye,
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Ernest Mangu
alisema mpango wa kuboresha jeshi hilo awamu
ya kwanza ulikuwa kwa miaka 10 kuanzia 2006
hadi 2014 lakini kulikuwa na changamoto
iliyoshirikisha Ofisi ya Rais na kutengeneza
mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) awamu
ya pili uliozinduliwa jana.
Alisema utekelezaji wake utaanza Julai Mosi,
mwaka huu kwa kuanza na wilaya ya Kinondoni na
baadaye kuenea nchi nzima kisha baada ya miaka
mitatu kufika maeneo yote ya nchi ambapo kwa
Jiji la Dar es Salaam zinahitajika Sh bilioni 27 ili
kuwa na hali ya usalama kuliko majiji yote Afrika.
Rais Magufuli alisema katika mpango huo
wataongeza ufanisi katika kushughulikia uhalifu
kwa kuwa na mtandao wa vituo vya Polisi
vikiwemo vya kuhamahama kwa kupeleka sehemu
uhalifu ulipokithiri na kuwa na askari wa doria
ambapo utaongozwa na GPS mpaka kituo kikubwa
cha mawasiliano.
Alisema pia kuboresha huduma za kipolisi na
kuboresha mawasiliano kwa kufungua kituo cha
mawasiliano kwa kuwasiliana na polisi wa doria ili
linapotokea tukio la uhalifu iwe rahisi kukabiliana
nalo kwa haraka na kubuni vyanzo vya fedha.
HabariLeo
Chapisha Maoni