0

KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van Pluijm
amesema timu yake bado ina nafasi ya
kupigania kufuzu hatua ya nusu fainali
ya michuano ya Kombe la Shirikisho
Afrika katika michezo mitatu iliyobaki.
Yanga iko kwenye nafasi mbaya ya
kusonga mbele kwenye michuano hiyo
baada ya kukosa matokeo mazuri katika
mechi tatu za mwanzo ambapo ilifungwa
na Mo Bejaia ya Algeria bao 1-0,
ikafungwa na TP Mazembe ya Congo DR
bao 1-0 na juzi ilitoka sare ya bao 1-1
na Medeama ya Ghana.
Akizungumza juzi baada ya mechi dhidi
ya Medeama, Pluijm alisema ni mapema
kukata tamaa kwani anaamini lolote
linawezekana kama timu yake
itapambana katika michezo iliyobaki na
hivyo kusonga mbele.
“Ni lazima tupambane na tushinde katika
michezo iliyobaki kujihakikishia nafasi ya
kusonga mbele. Hatuwezi kukata tamaa
kwa matokeo yaliyopita, kwani lolote
linawezezekana,” alisema.
Akizungumzia mchezo wa juzi, Pluijm
alisema alijua mapema kuwa Medeama
ni timu nzuri na yenye nguvu, kwani
walicheza vizuri. Kwa upande wa timu
yake, alisema ilicheza vizuri ingawa
muda mwingi ilikuwa ikitumia kupiga
mipira mirefu na kushindwa kucheza
mchezo wa pasi waliouzoea kutokana na
presha
. “Tulitarajia kushinda lakini soka ni
mchezo wa makosa ukishindwa kufunga
unakuwa kwenye wakati mgumu,”
alisema na kuongeza kuwa bado kuna
tatizo linalojirudia la kutengeneza nafasi
na kushindwa kufunga.
Alisema walikuwa kwenye hatari ya
kupoteza mechi hiyo dakika za mwisho
za mchezo kwa kuwa Medeama walipata
nafasi moja wakaipoteza. Kwa upande
wake kocha wa Medeama, Pride Owusu
alisema kikosi chake kilicheza vizuri na
kwamba moja ya malengo yao ilikuwa ni
kushinda au kutoka sare hivyo
wamefurahia matokeo.
Alisema siri ya kuibana Yanga ni kwa
vile walipata video zao na kuzifanyia
kazi ambapo walifanikiwa na hivyo
wanarudi kwao kujipanga katika michezo
iliyobaki ili kufanya vizuri.
“Tunashukuru kwa matokeo haya, kikosi
changu kilicheza vizuri tunarudi
nyumbani kujipanga katika michezo
iliyobaki, uwezo wa kufuzu nusu fainali
tunao,” alisema.
Yanga itaendelea kushika nafasi ya
mwisho kwenye kundi A ikiwa na pointi
moja ikifuatiwa na Medeama yenye pointi
mbili, Mazembe na Mo Bejaia
waliotarajiwa kumenyana jana ndio
wanaongoza kwenye kundi hilo.



Posted Africa News Sports

Chapisha Maoni

 
Top