0
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema kupungua kwa mizigo bandarini kumeathiri si Tanzania pekee bali dunia nzima na kwamba
kubanwa kwa mianya ya wizi kumesababisha
kuongezeka kwa mapato kutoka Sh bil 458 Aprili
mwaka huu kufikia Sh bil 517.
Aidha, TRA imesema itaanza uhakiki wa namba za
utambulisho wa mlipakodi (TIN) kutokana na
kuwepo watu wenye namba mbili na wasiohakiki
watalazimika kudaiwa kodi na TRA.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari jana,
Kamishna wa TRA, Alphayo Kidata alisema
upungufu huo wa mizigo bandarini umezikumba
pia bandari za Beira, Msumbiji, Mombasa, Kenya
na kwingineko na kusababisha mapato kupungua.
“Lakini sisi pamoja na upungufu wa mizigo
bandarini makusanyo yanazidi kuongezeka
kutokana na kuzibwa mianya ya kukwepa kodi,
hivyo napenda kuwapongeza wafanyakazi wote
wa mamlaka na kusema kwa sasa hakuna mtu
anayeweza kukwepa kodi na wale waliozoea
wakae katika njia kuu,” alisema Kidata.
Kidata alisema wananchi wanatakiwa kuwaunga
mkono kwani sasa kodi inaonekana katika
kufanya shughuli za serikali kama kuboresha
miundombinu pamoja na kutoa elimu bure.
Alisema TRA imefikia na kuvuka lengo la
makusanyo ya kodi kwa mwaka wa fedha
2015/16 kwa kukusanya Sh trilioni 13.8 sawa na
asilimia 100.04 ya lengo la kukusanya Sh trilioni
13.4 iliyokuwa imepangwa na serikali.
Kidata alisema katika kipindi cha Juni mwaka
huu, TRA imekusanya Sh trilioni 1.4 sawa na
asilimia 107.83 ya lengo la kukuzanya Sh trilioni
1.3 ambapo makusanyo ya mwaka wa fedha
2015/16 ni sawa na ongezeko la asilimia 23.70 la
makusanyo ya mwaka 2014/15.
Akizungumzia mashine za kielektroniki za EFDs,
Kidata alisema walipoanza utoaji mashine hizo
zilikuwa 5,703 na mpaka sasa mashine 1,700
zimegawiwa kwa watumiaji na wataanza kupita
duka hadi duka kuhakiki matumizi ya mashine
hizo.
Kamishna wa mapato ya ndani, Elijah
Mwandumbya, alisema mwaka huu wa fedha
wamejipanga kuhakikisha wanaondoa
changamoto kwa mtu mmoja kuwa na TIN zaidi
ya moja hivyo watafanya uhakiki.

Chapisha Maoni

 
Top