Jose Mourinho ametoa ishara kubwa kwamba zile
tetesi za Timu yake Manchester United kumsaini
tena Kiungo wa France Paul Pogba kutoka
Juventus zina ukweli aliposema: "Kukiwa na
moshi, kuna moto!"
Zipo ripoti kuwa Man United wameshaafikiana na
Juve kulipa Dau la Rekodi ya Dunia la Pauni
Milioni 100 kumnunua Pogba, mwenye Miaka 23,
alieondoka Man United kwenda Juve Mwaka 2012
bila Ada yeyote ile zaidi ya kulipwa Fidia ya
kukuza kipaji ya Pauni 800,000 tu.
Mourinho pia amesema: "Nitakuwa mpuuzi kama
pia sitasema tunajaribu kwa zaidi ya Mchezaji
mmoja!"
Katika Kipindi hiki, Mourinho ameshasaini
Wachezaji Watatu Wapya ambao ni Eric Bailly
kutoka Villarreal, Henrikh Mkhitaryan wa Borussia
Dortmund na Zlatan Ibrahimovic.
Alipoulizwa kuhusu kumsaini Pogba, Mourinho
alijibu: "Tulilenga Mtu 4 na tumepata watatu na
tutampata wa nne. Tuliamua Wanne ili kuboresha
Kikosi kitupe uwezo wa kuwa na aina nyingi
tofauti, kicheze kama ninavyolifikiria Soka."
Aliongeza: "Kila Mtu anamfikiria mmoja lakini
haitanishangaza kama sio yeye na ni mwingine!"
Kuhusu Wayne Rooney, ambae amebakiza Bao 4
tu kuikamata Rekodi ya Sir Bobby Charlton
aliefunga Bao 249 ambazo ni nyingi katika
Historia ya Man United, Mourinho ameeleza:
"Nashangaa kuhusu maswali mengi kuhusu huyu
jamaa. Yeye ni Kepteni wa Klabu, ni Kepteni wa
Meneja, ni Kepteni wa Wachezaji. Namwamini
sana. Nadhani atakuwa Mchezaji muhimu
kwangu!"
Mara mbili akiwa na Chelsea Mourinho alitoa Ofa
za kumnunua Rooney na zote kukataliwa na Man
United.
Kuhusu Juan Mata ambae aliuzwa na Chelsea
kwenda Man United Mwaka 2014 kwa Dau la
Pauni Milioni 37.1, Mourinho amesema ipo nafasi
kwa Mata kubaki kwenye Timu na kupigania
nafasi.
Mourinho alifunguka: "Kwanza bora niweke
mambo sawa kuhusu Klabu yetu iliyopita kwa
sababu sikwambia Mata aondoke. Sikulazimisha
auzwe. Ulikuwa uamuzi wake binafsi kuhama na
mimi sipendi Wachezaji kuondoka. Kama
Mchezaji hataki kubaki nasi basi kwa heri. Lakini
nadhani sasa ana furaha na sidhani kama
ataomba kuondoka."
Posted Africa News Sports
Chapisha Maoni