Klabu ya mpira wa miguu ya Ruvu Shooting
ya mkoani Pwani, inayoshiriki ligi kuu ya
Vodacom Tanzania bara(VPL) imetamba
kufanya makubwa msimu ujao wa Ligi hiyo
na kuwataka mabingwa wa ligi hiyo, Yanga
kutarajia upinzani mkali kutoka kwao
katika kupigania taji hilo.
Akizungumza kutoka Mlandizi yalipo
maskani ya timu hiyo, Ofisa Uhusiano wa
Ruvu Shooting, Masau Bwire, alisema kuwa
malengo yao msimu ujao ni kuwa miongoni
mwa timu tatu za juu na ikiwezekana
kutwaa ubingwa kama walivyofanya
Leicester City ya England ambayo msimu
uliopita ilipanda daraja na kubeba taji.
Alisema kuwa kikosi chao kipo katika
maandalizi kabambe na kwamba Jumatatu
wanatarajia kutambulisha wachezaji wao,
wakati watakapovaana na Mbeya City
katika mchezo wa kirafiki utakaopigwa
kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi.
“Baada ya kupanda daraja, matarajio yetu
ni kucheza kandanda maridadi kama ilivyo
kawaida yetu, lakini pia kupambana ili
tuweze kuwa katika nafasi za juu, hivyo
hizo timu zinazojiita kubwa, yaani Simba
na Yanga, zikae chonjo,” alisema Bwire.
Alisema kwamba kwa jinsi wanavyojipanga,
iwapo waamuzi watazingatia sheria zote 17
za soka, ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom
msimu ujao lazima utue Mlandizi yalipo
maskani yao.
Akiuzungumzia udhamini wa ligi hiyo,
alisema angalau unawasaidia kufanikisha
ushiriki wao wa ligi hiyo kwenda vizuri,
japo wamekuwa wakikabiliana na
changamoto mbalimbali.
Aliipongeza kampuni ya Vodacom Tanzania
ambao ni wadhamini wa ligi hiyo kwa
kuendelea kudhamini ligi hiyo na kuboresha
sehemu ya udhamini wao kila mara,Pia
aliitaka kampuni hiyo kuangalia kama
wanaweza si tu kuwahisha kuwapa fungu
la maandalizi ya ligi, lakini pia kuongeza
kiwango zaidi kwa mkataba ujao ili timu
nyingi zinazoshiriki ligi hiyo zisiwe
zinapata usumbufu wa kujiendesha.
Posted Africa News Sports
Chapisha Maoni