0
SERIKALI imemtaka Mkurugenzi wa Mashtaka
(DPP) kuchukua hatua stahiki katika shauri la kesi
ya jinai namba 100 ya Jamhuri dhidi ya Isaac
Emily aliyeadhibiwa kulipa faini kwa kumtukana
Rais John Magufuli mtandaoni.
Hayo yamesemwa jana bungeni na Waziri wa
Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe wakati
akitoa kauli ya serikali baada ya mwongozo
ulioombwa na wabunge wa CCM, Juma Nkamia
wa Jimbo la Chemba na Livingstone Lusinde wa
Mtera, baada ya hukumu hiyo kutolewa hivi
karibuni. Hata hivyo, hatua stahiki hizo
hazikuelezwa.
Alisema nia ya maagizo hayo kwa DPP ni kulinda
dhana na dhamira ya adhabu katika mfumo wa
haki jinai ambayo hutaka mhukumiwa kujutia
kosa lake na wengine kujifunza kutoka kwake.
Katika maelezo yake, Waziri Mwakyembe alisema
kwa hali ilivyo katika shauri hilo, dhana na
dhamira ya adhabu haikuweza kufikiwa kwa
mwenendo wa kuingiza siasa katika utekelezaji
wa hukumu.
Alisema serikali imejiridhisha na kilichotokea
katika shauri hilo na kauli za wabunge walioomba
mwongozo kwamba masharti ya adhabu yalikuwa
mepesi mno usiolingana na shauri lenyewe.
Alisema aliyehukumiwa analifanyia siasa suala
hilo na kuigeuza adhabu rafiki aliyopewa kuwa
burudani ya kisiasa katika mitandao ya kijamii.
“Mheshimiwa spika, nimejiridhisha na
kilichotokea. Madhara ya mwelekeo huu mpya
katika haki jinai, ni kuchochea vitendo zaidi vya
ukaidi kwa mamlaka za nchi na hivyo kujenga
msingi wa vurugu. Hili halikubaliki katika utawala
wa sheria. Mdharau mwiba mguu huota tende,”
alisema..
Alisema kosa kama hilo lilitokea Kenya mwaka
jana ambapo mwanafunzi wa Chuo Kikuu nchini
humo, Alan Okengo (25) alihukumiwa kifungo cha
mwaka mmoja na kulipa faini ya dola 2,000 (Sh
milioni 3.2) kwa kumtukana rais wa nchi hiyo
kwenye mitandao ya kijamii.
Alisema pamoja na umri wake na uwezo wake
mdogo wa kulipa faini, adhabu ilibaki palepale ili
mkosaji ajutie kosa lake asije akarudia na jamii
ijisikie salama.
Alisema pamoja na kutokuingilia mhimili wa
mahakama na taratibu zake kitendo cha kuwapo
kwa adhabu ambayo haijutiwi inakiuka dhana na
dhamira ya adhabu.
Alisema kwa shauri la Emily, pamoja na kutiwa
hatiani wakili wake aliomba mtuhumiwa alipe faini
kwa kuwa hakusumbua mahakama na pia ni kosa
lake la kwanza na ana familia.
Alisema wakati hakimu anamuuliza wakili wa
serikali aliiachia mahakama kutoa maamuzi
ambayo ilimpatia wakili wa utetezi maombi yake.
Mwakyembe alisema pamoja na maagizo ya
serikali kwa DPP amewakumbusha waendesha
mashitaka nchini kuwa macho na waweke mbele
weledi na maslahi mapana ya taifa na kamwe
wasiyumbishwe na mihemko ya kisiasa katika
jamii.

Chapisha Maoni

 
Top