Mipango ya kukabiliana na "tabia isiyovumilika" ya
wachezaji na mameneja katika soka la England
imetangazwa. Katika taarifa iliyotolewa na Ligi Kuu,
Ligi nyingine na Chama cha soka cha England,
imesema nidhamu mbaya imefikia "viwango
visivyokubalika". Kuanzia msimu huu, kadi
nyekundu zitatolewa kwa wachezaji watakaomkabili
mwamuzi au kutumia lugha za matusi au hata kwa
ishara. Nidhamu pia katika 'benchi la ufundi'
itazingatiwa. Hakuna mchezaji hata mmoja katika
Ligi Kuu ya England alioneshwa kadi nyekundu
kwa kumtukana au kutumia lugha chafu kwa
mwamuzi katika misimu mitano iliyopita. Lakini
mwenyekiti wa Ligi Kuu, Richard Scudamore
amesema kumekuwa na wasiwasi "kwa muda
sasa" kuwa wachezaji wamekuwa "wakivuka
mipaka". "Kwa pamoja tumeona tabia hii haitakiwi
kuendelea kuvumiliwa," amesema Scudamore.
"Matukio yanatokea kwa haraka sana kwenye
mchezo wenye mvutano mkali. Bado tunataka
kuona ari ambayo mashabiki watafurahia, lakini
wachezaji na mameneja watatakiwa kuwa makini
kuwa hawavuki mipaka."
Makosa yanayoweza kusababisha kadi ya manjano:
Kuonesha nidhamu mbaya waziwazi kwa mwamuzi
yoyote;
Kubishia uamuzi kwa ghadhabu;
Kumkabili mwamuzi uso kwa uso;
Kumkimbilia mwamuzi kubisha kuhusu uamuzi
uliotolewa;
Lugha ya matusi, lugha chafu au ishara za matusi
dhidi ya waamuzi;
Kumgusa mwamuzi yoyote bila ya ghadhabu
kupinga uamuzi;
Kadi ya manjano kwa angalau mchezaji mmoja
pale mchezaji mmoja au zaidi watamzonga na
kumzunguka mwamuzi.
Makosa ya kadi nyekundu:
Iwapo mchezaji atamkabili mwamuzi na kutumia
lugha ya matusi au kutumia ishara.
Kumgusa mwamuzi kwa ghadhabu kupinga
uamuzi.
Posted Africa News Sports
Chapisha Maoni