0
YANGA SC itaendelea
kumkosa mshambuliaji wake
Mrundi, Amissi Tambwe
katika mchezo wa leo dhidi
ya Mouloudia Club Alger ya
Algeria.
Mabingwa hao wa Tanzania,
wanateremka Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam
kumenyana na timu kutoka
Algeria katika mchezo wa
kwanza wa mchujo kuwania
kuingia hatua ya makundi ya
Kombe la Shirikisho Afrika.
Tambwe aliyekuwa
anasumbuliwa na maumivu
ya goti tangu Januari,
amepona na ameshiriki
mazoezi na wenzake kwa
wiki yote hii, lakini ameomba
wiki moja zaidi ili awe fiti
kikamilifu kabla ya kurejea
kuipigania timu yake kwenye
vita ya mataji.
Amissi Tambwe (kushoto)
amefanya mazoezi wiki yote
hii, lakini hayuko tayari kwa
mchezo wa leo
MC Alger wamefanya
mazoezi Uwanja wa Taifa
jana baada ya kuwasili
Alhamisi
Pamoja na Tambwe, Yanga
itaendelea kumkosa kiungo
Mzambia, Justin Zulu
aliyeumia ugoko baada ya
kugongwa na Himid Mao wa
Azam Aprili 1, ambaye
anatarajiwa kufunguliwa
nyuzi kesho kabla ya kuanza
mazoezi Jumatatu, maana
yake anaweza kuwa fiti kwa
mchezo wa marudiano Aprili
15 mjini Algiers.
Lakini habari njema ni
kwamba Wazimbabwe wawili
waliokuwa majeruhi, kiungo
Thabani Kamusoko na
mshambuliaji Donald Ngoma
wamepona na leo wanaweza
kucheza.
Mchezo huo unaotarajiwa
kuanza Saa 10:00 jioni,
utachezeshwa na marefa
kutoka Rwanda, Louis
Hakizimana atakayepuliza
filimbi akisaidiwa na washika
vibendera Theogene
Ndagijimana na Jean Bosco
Niyitegeka, wakati refa wa
akiba atakuwa Ruzindana
Nsoro na Kamisaa ni Ata
Elmanan Hassan Osama
kutoka Sudan.
Yanga wamekuwa katika
maandalizi ya mchezo huu
kwa wiki nzima tangu
waifunge Azam 1-0 kwenye
mchezo wa Ligi Kuu
Jumamosi iliyopita, bao
pekee la Mzambia, Obreu
Chirwa Uwanja wa Taifa.
Wakati Yanga imeweka kambi
katika hoteli ya Tiffany
makutano ya barabara ya
Morogoro na Mtaa wa Indira
Gandhi, wapinzani wao MC
Alger waliwasili juzi Saa 3.30
usiku kwa ndege maalumu
ya kukodi na kufikia Hoteli ya
Holiday Inn, katikati ya Jiji.
Jana jioni Waarabu hao
walifanya mazoezi Uwanja wa
Taifa na wachezaji wake
walionekana wachangamfu
pamoja na hali ya baridi na
mvua za rasha rasha.
Viingilio katika mchezo huo
ni Sh 30,000 kwa VIP ‘A’; Sh
20,000 kwa VIP ‘B’ na ‘C’
wakati mzungunguko itakuwa
ni Sh 3,000.
Wakati Yanga SC, imeangukia
kwenye kapu la kuwania
kucheza hatua ya makundi ya
Kombe la Shirikisho baada
ya kutolewa na Zanaco ya
Zambia katika Ligi ya
Mabingwa, MC Alger imefika
hatua hii kwa kuitoa
Renaissance ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo
(DRC).
Hatua hii hukutanisha timu
zinazotolewa Ligi ya
Mabingwa dhidi ya
zinazofuzu hatua ya 32 Bora
Kombe la Shirikisho na
Yanga ililazimishwa sare ya
1-1 Dar es Salaam kabla ya
kutoa sare ya 0-0 Lusaka,
hivyo kutolewa kwa mabao
ya ugenini, wakati MC Alger
ilishinda 2-0 nyumbani na
kwenda kufungwa 2-1
Kinshasa, hivyo kufuzu kwa
ushindi wa jumla wa 3-2.
Mwaka jana pia Yanga
ilitolewa na Al Ahly ya Misri
katika hatua ya 16 Bora ya
Ligi ya Mabingwa na
kuangukia kwenye kapu la
kuwania kucheza hatua ya
makundi ya Kombe la
Shirikisho, ambako iliitoa
Sagrada Esperanca ya
Angola.
Kila la heri wawakilishi pekee
wa Tanzania waliobaki katika
michuano ya Afrika. Mungu
ibariki Yanga. Mungu ibariki
Tanzania. Amin.

Chapisha Maoni

 
Top