0

Mahakama ya hakimu Mkazi Kisutu imewanyima dhamana Rais wa TFF Jamal Malinzi, Katibu Mkuu Mwesigwa Celestine na Mkurugenzi wa Fedha wa TFF Nsinde Isawale Mwanga, kwa kuwa tuhuma zinazowakabili za kutatikisha fedha hazina dhamana.
Malinzi, Mwesigwa na Nsinde, wanashtakiwa kwa makosa 28 ambayo ni kughushi nyaraka mbalimbali na kutakatisha fedha, ambapo Kesi yao ilitajwa kwa mara ya kwanza June 29 mwaka huu, ambapo upande wa utetezi uliwasilisha maombi mawili.
Ombi la kwanza ni kuiomba mahakama kuanza kusikiliza kesi hiyo kwani upande wa mashtaka ina ushahidi hivyo haioni sababu ya kutoanza kusikilizwa kwa madai upelelezi haujakamilika huku Ombi la pili likawa ni dhamana kwa watuhumiwa.
Hakimu Mkazi Wilbroad Mashauri aliaghirisha kesi hiyo, hadi July 03 kwa ahadi kuwa angetoa hukumu ya maombi ya hayo.
Akianza na ombi la kwanza Hakimu Mashauri ametupilia mbali ombi la kuanza kusikiliza kesi hiyo kwani sheria inawaruhusu upande wa mashtaka kupeleka kesi mahakamani hata kama ushahidi haujakamilika.
Kuhusu Upelelezi.
Hakimu Mashauri akaongeza kuwa sheria inawaruhusu upande wa mashtaka kufanya upelelezi ndani ya siku tisini tangu kesi kutajwa kwa mara ya kwanza, huku akiusisitiza upande huo unaowakilishwa na Mawakili wa TAKUKURU kukamilisha upelelezi wao ndani ya siku hizo.
Kuhusu Ombi la dhamana, hakimu ametupilia mbali ombi hilo kwa maelezo kuwa kesi zinazowakabili washtakiwa hao za kutakatisha fedha hazina dhamana.
Baada ya kutoa hukumu hizo Hakimu Wibroad Mashauri akaghairisha kesi hiyo hadi Julai 17 mwaka huu hivyo Malinzi, Mwesigwa na Nsinde wamerudishwa rumande.


Chapisha Maoni

 
Top