Mabingwa wa Tanzania Bara, timu ya soka ya Dar Young Africans wamefanikiwa kutinga katika hatua ya kwanza ya michuano ya klabu bingwa barani Afrika baada licha ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya St Louis United ya Shelisheli.
Wakicheza kandanda safi katika uwanja wa Stade Linite uliopo mjini Victoria, Yanga walipata bao la kwanza dakika moja tu kabla ya kwenda mapumziko kupitia kwa Ibrahim Ajib.
St Louis walipata bao la kusawazisha katika dakika ya 90 baada ya walinzi wa Yanga kufanya uzembe na kumruhusu mchezaji wa St Louis kupiga free header na mpira kujaa wavuni.
Yanga wanafuzu Hatua inayofuata kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya mchezo wa duru ya kwanza kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 mchezo ambao ulifanyika nyumbani jijini Dar es Salaam.
Kwa sare hiyo sasa Yanga watakutana na mshindi wa mchezo kati ya El Merreikh ya Sudan na Township Rollers ya Botswana mchezo ambao utafanyika siku majira ya saa 2:30.
Kikosi kilichoanza: Rostand Youthe, Ramadhan Hamis Kessy, Gadiel Michael Mbaga, Nadir Haroub Canavaro, Kelvin Yondani, Said Juma Makapu, Pato Ngonyani, Pappy Kabamba Tshishimbi, Pius Buswita, Ibrahim Ajib Migomba na Emmanuel Martin.
Akiba: Ramadhan Kabwili, Juma Abdul Jaffary, Mwinyi Haji Mngwali, Yussuf Mhilu Said Mussa Ronaldo, Raphael Daudi Loth na Geofrey Mwashiuya.
JKU na Zimamoto
Wakati huohuo timu zote kutoka Zanzibar zimeondolewa kwenye mashindano ya kimataifa baada ya kukubali vichapo ugenini.
Waliokuwa wakishiriki mashindano ya klabu bingwa Afrika timu ya soka ya JKU wameondolewa kwa aibu, baada ya kukubali kichapo cha mabao 7-0 Kutoka kwa Zesco United.
Mchezo huo umefanyika katika uwanja wa Levy Mwanawasa mjini Ndola, Zambia huku mchezaji Adam Zikiru akifunga mabao manne pekee yake.
Wakati wenzao wa Zimamoto wametolewa kwa jumla ya mabao 2-1 na Welayta Dicha ya Ethiopia katika mchezo wa duru ya pili ya michuano ya kombe la Shirikisho Afrika.
Katika mchezo wa awali uliofanyika mjini Unguja timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 huku mchezo huo wa duru ya pili ukimalizika kwa Zimamoto kufungwa bao 1-0.
Chapisha Maoni