KIUNGO mchezeshaji wa Simba Mnyarwanda, Haruna Niyonzima ni kama ameikacha kiaina kambi ya timu hiyo ni baada ya viongozi kulalamika kutopokea simu kila wakimtafuta hewani.
Kiungo huyo alitakiwa kuwepo kwenye msafara wa wachezaji wanne waliosafiri juzi kuelekea Uturuki kujiunga na wenzao lakini hakuwepo huku wenzake, Said Ndemla, Hassani Dilunga, Meddie Kagere na Erasto Nyoni wakiwa wametua na kuanza kujifua.
Mnyarwanda huyo alijiunga na Simba kwenye msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara akitokea Yanga baada ya mkataba wake kumalizika wa miaka miwili.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi,
kiungo huyo bado yupo nyumbani kwao Rwanda alipokwenda kwenye mapumziko, hivyo bado hajajiunga na kambi ya Uturuki kama inavyoelezwa.
Mtoa taarifa huyo alisema, kiungo huyo alitakiwa kuripoti Dar wiki moja iliyopita kabla ya timu kuelekea Uturuki, lakini alikaidi agizo alilopewa na uongozi na sababu ni kibali chake cha kuisafiria ‘paspoti’ kumalizika.
“Awali, Niyonzima alituambia kuwa paspoti yake imemalizika tukamuambia atutumie kwa ajili ya kumtengezea mpya akatutumia, lakini tangu alipotutumia ikawa kimya.
“Tumejaribu kumtafuta mara kwa njia ya simu kwa kumpigia wakati mwingine simu inaiita lakini haipokelewi, tukimtafuta wakati mwingine simu yenyewe haipatikani, hivyo tunashindwa kumuelewa.
“Inavyoonekana kama hataki kujiunga na kambi ya Uturuki, hivyo kama uongozi tumeona tuachane naye atakapojisikia kujiunga na timu atakuja kwa sababu yeye anafahamu kabisa timu ipo kwenye ‘pre season’ alitakiwa kuwa na timu pamoja,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Niyonzima kuzungumzia hilo simu yake mkononi ilikuwa haipatikani na alipotafutwa kwa njia ya mtandao wa kijamii wa ‘WhatsAp’ meseji yake haikufika kujibu hilo.
Chapisha Maoni