LIGI Kuu England imebakiza siku 13 tu kabla ya kuanza. Kila timu inajaribu kuunda kikosi chake imara kabisa kuhakikisha msimu ujao unakuwa bora upande wake na ikiwezekana kuubeba ubingwa wenyewe kabisa.
Lakini kwenye Top Six kama ilivyo kwa sasa, kila timu hapo inahitaji kufanya usajili mmoja muhimu kabla ya dirisha la kusajili halijafungwa, Agosti 9.
Hizi ndizo nafasi ambazo Top Six wote wanapaswa kusajili kabla ya dirisha hili kufungwa.
Arsenal - mshambuliaji
Arsenal ya mwaka huu ni matata kwelikweli, kocha wake, Unai Emery hakutaka mchezo katika kuhakikisha anafanya usajili mapema na kuifanya timu yake kuja na nguvu mpya kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu England.
Usajili mpya umeonekana kuimarisha zaidi ngome ya ulinzi, kwani amesajili mabeki wawili, kipa na kiungo wa kukaba. Kwenye nafasi ya viungo wa kati na wale wa kushambulia si tatizo, kwa sababu katika nafasi hiyo kuna wakali wengi tu akiwamo Henrikh Mkhitaryan, Mesut Ozil, Alex Iwobi na wengineo.
Shida ipo sehemu moja tu, Arsenal inahitaji mshambuliaji mwingine wa kiwango cha dunia ili kushindania nafasi na wakali kama Pierre-Emerick Aubameyang na Alexandre Lacazette.
Arsenal inahitaji kuwa na mtu anayeweza kutumia nafasi kwa ufasaha zaidi, nafasi moja bao moja.
Chelsea - mshambuliaji
Kuhusu Chelsea hali yake ya nani aje kwenye kikosi itategemea zaidi na atakayeondoka. Lakini, kama mambo yatabaki kama yalivyo, basi wababe hao wa Stamford Bridge watahitaji kusajili mshambuliaji wa kati.
Pengo la Nemanja Matic imeshaliziba kwa kumsajili Jorginho, ambaye atakiwasha kwenye sehemu ya katikati ya uwanja. Lakini, mtihani unaoikabili upo kwa wachezaji Eden Hazard na Thibaut Courtois, wanaowindwa mchana usiku na Real Madrid.
Kikosi chake kina washambuliaji Alvaro Morata, Michy Batshuayi na Olivier Giroud, lakini wakali hao si watu wa kuwaamini sana, wanafunga leo kisha wanasubiri mechi kibao bila ya kufunga. Kuondokana na hilo, Chelsea inahitaji kusajili mshambuliaji atakayewahakikishia mabao.
Liverpool - beki wa kati
Hii ni habari ambayo Dejan Lovren hatapenda kabisa kuisikia Liverpool bado inahitaji beki mwingine wa kati.
Ishu ni hivi, beki huyo wa kati mpya akija, Lovren ndiye mtu atakayekuwa kwenye benchi kwa sababu Jurgen Klopp hataweza kumweka beki wake ghali, Virgil van Dijk kwenye benchi.
Joel Matip ameumia na Joe Gomez si beki wa kumtegemea sana hasa kwa Liverpool ya msimu huu ambayo imelenga kufanya mambo makubwa kwenye Ligi Kuu England.
Maeneo mengine Liverpool inaonekana kuwa imara hasa ukizingatia hata kwenye goli imemsajili kipa makini kabisa, Alisson Becker, hivyo inahitaji beki wa kati wa kuwafanya wawe imara zaidi.
Kutokana na hilo ndio wababe hao wa Anfield wamekuwa wakihusishwa na mpango wa kumsajili beki wa kati wa Croatia, Domagoj Vida.
Man City - kiungo wa kati
Kutaka pengine utaonekana ni msamiati wa kushtukiza kwa Manchester City, kwa sababu kikosi chake kina kila kitu na kimesheheni kila idara kikiwa na wachezaji makini kwelikweli, kila kwenye eneo kukiwa na wachezaji wawili waliokwenye ubora mkubwa.
Benjamin Mendy amepona, hivyo atarudi kwenye nafasi yake na Fabian Delph ataanza kutumia kwenye nafasi yake ya asili, kiungo wa kati.
Kyle Walker, ambaye amekuwa akitumika kama beki wa pembeni, anaweza kucheza beki wa kati pia, hivyo jambo hilo linaifanya Man City kutompa presha kubwa kocha wake, Pep Guardiola.
Lakini linapokuja suala la mahitaji ya kuwa na kikosi chenye mastaa makini zaidi, Guardiola anahitaji kuwa na huduma bora ya mchezaji atakayekuja kusaidiana na Fernandinho kwa sababu Mbrazili huyo akipata majerahi tu, itakuwa majanga.
Kutokana na hilo, ndiyo Guardiola alikuwa akiwasaka Fred na Jorgonho, ambao wote hao amewakosa, mmoja akienda Manchester United na mwingine Chelsea.
Man United - beki wa kati
Ukikaa na Jose Mourinho lazima atakushangaza kwa maneno yake kwamba atahitaji wachezaji wengine 11.
Lakini, hayo ni maneno yake tu ya kutaka kuwazidi maarifa wapinzani wake. Mourinho anafahamu wazi kama kuna eneo ambalo anapambana nalo kwa nguvu zote kufanya usajili kwenye dirisha hili, basi ni beki wa kati. Kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi, amesajili kiungo Fred na beki wa pembeni, Diogo Dalot.
Eneo ambao anataka kusajili mchezaji mwingine ni kwenye winga na hilo kama tu wengine wataondoka, lakini piga ua, beki wa kati ndicho kitu kinachomnyima usingizi Mreno huyo.
Man United imekuwa na orodha ndefu ya mabeki wa kati inaowafukuzia akiwamo Toby Alderweireld wa Tottenham na Harry Maguire wa Leicester City.
Kuna wakati ilihusishwa pia na mpango wa kumnasa Raphael Varane wa Real Madrid.
Tottenham - kiungo mshambuliaji
Hakuna mabadiliko makubwa kwenye kikosi cha Tottenham Hotspur. Hakuna mchezaji aliyeondoka, hivyo haina presha kubwa ya kutafuta wacheza mbadala wa kuziba mapengo.
Wachezaji wanaotia presha ya kuondoka ni Toby Alderweireld, Danny Rose na Mousa Dembele. Lakini iwe kuna mchezaji ameondoka au hakuondoka, Spurs inahitaji kufanya usajili mwingine wa kiungo mshambuliaji ili kuifanya kuwa na chaguo mbadala baada ya Christian Eriksen.
Ni jambo la bayana kabisa Kocha Mauricio Pochettino anakuwa kwenye mtihani mzito pindi anakosa huduma ya Eriksen kwa sababu ndiye mchezaji anayeifanya safu ya ushambuliaji ya kina Dele Alli na Harry Kane kutulia na kufunga mabao.
Chapisha Maoni