Klabu ya Liverpool, imemaliza mechi za kujipima nguvu ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu mpya kwa ushindi wa kishindo wa mabao 3-1 dhidi ya Torino ya Italia, mchezo uliochezwa jana usiku dimbani Anfield.
Kiungo Fabinho, alishindwa kuifungia Liverpool bao la kuongoza alipokosa mkwaju wa penalti iliyotokana na Sadio Mane kuangushwa ndani ya eneo la hatari.
Kocha Jurgen Klopp, ambaye alikianzisha kikosi imara alifurahia pale kiungo wake Roberto Firmino akiifungia timu yake bao la kuongoza mapema kabla ya nyota huyo kutoka Brazil kufunga la pili ndani ya dakika 45.
Kiungo wa Kiholanzi Georginio Wijnaldum aliifungia Liverpool bao la tatu huku kipa mpya wa timu hiyo mbrazil, Alisson akionekana kufanya vizuri langoni, mpira pekee uliomshinda kuudaka ni ule wa kichwa uliopigwa na Andrea Belotti aliyeifungia Torino bao la kufutia machozi.
Ushindi huo unawaweka Liverpool katika hali nzuri wanapoisubiri West Ham United katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu England mchezo utakaopigwa Anfield.
Kocha Klopp anasubiri kuona kiwango cha wachezaji wake waliokuwa majeruhi kwa kipindi kirefu msimu uliiopita na nyota wapya ambao sasa wapo fiti ambao ni Daniel Sturridge, Adam Lallana, Danny Ings na Marko Grujic, mchezaji mpya ni Xherdan Shaqiri.
Maria Sharapova apeta Rogers Cup
Montreal, Canada. Mcheza tenisi mahiri wa Russia, Maria Sharapova, amerejea katika kiwango chake bora baada ya jana kumng’oa Sesil Karatantcheva wa Bulgaria, katika michuano ya Rogers Cup.
Sharapova alimshinda Sesil Karatantcheva kwa seti mbili za 6-1, 6-2 ikiwa ni mara yake ya kwanza kushiriki mashindano ya Rogers Cup tangu mwaka 2014.
Naye mchezaji Eugenie Bouchard wa Canada anayeshika nafasi ya 129 kwa ubora duniani alishinda kwa 6-2, 6-4 Elise Mertens wa Ubelgiji.
Hata hivyo Bouchard, aliumia kidole gumba cha mguu na kuomba mchezo usimamishwe ili atibiwe na baadaye kumalizia mchezo huo huku akichechemea.
Katika mchezo uliochezwa mapema Jelena Ostapenko wa Lativia alishindwa kuwika mbele ya Mwingereza Johanna Konta alipochapwa kwa 6-7 (6), 6-1, 6-2.
Naye Kiki Bertens wa Uholanzi alimshinda Carol Zhao wa Canada, akimchapa kwa 6-1, 6-2 wakati Petra Kvitova alimshinda Anett Kontaveit wa Estonia kwa 6-3, 6-4.
Aidha mchezaji Alison Van Uytvanck wa Ubelgiji alimshinda Sofya Zhuk wa Russia kwa 6-1, 6-2 huku Sorana Cirstea akimshinda Monica Niculescu kwa 3-6, 6-4, 6-4 ukiwa ni mchezaji uloiowakutanisha wachezaji wote kutoka nchini Romania.
Mcheza tenisi mahiri wa Ujerumani, Julia Goerges naye alimshinda Lucie Safarova kwa 2-6, 6-4, 6-3, huku Victoria Azarenka wa Belarus akimshinda Mfaransa Kristina Mladenovic kwa 6-0, 6-1 na Caroline Garcia alimshinda Magdalena Rybarikova wa Slovakia kwa 4-6, 6-1, 6-3.
Chapisha Maoni