Makundi ya Europa League
baada ya kupangwa Mshambuliaji wa Tanzania, Mbwana Samatta atakuwa na kazi nyepesi katika Europa League baada ya timu yake, KRC Genk kupangwa Kundi I pamoja na Besiktas ya Uturuki, Malmo FF ya Sweden na Sarasporg FC ya Norway.
Katika droo ya hatua ya makundi iliyopangwa leo ukumbi wa Grimaldi Forum mjini Monaco, Ufaransa, vigogo wa England, Arsenal wamepangwa Kundi E pamoja na Sporting Lisbon, Qarabag na Vorskla Poltava.
Chelsea wao wamepangwa Kundi L pamoja na PAOK, BATE Borisov na Vidi wakati moja ya vigogo wa Ulaya, AC Milan ya Italia imepangwa Kundi F pamoja na Olympiacos, Real Betis na Dudelange ya Luxembourg.
Samatta jana alikamilisha mchango mzuri kwa timu yake, KRC Genk kutinga hatua ya makundi y Europa League baada ya kufunga bao la nne katika ushindi wa 4-2 dhidi ya wenyeji, Broendby IF Uwanja wa Broendby nchini Denmark.
Genk imetinga hatua ya makundi kwa ushindi wa jumla wa 9-4 baada ya kushinda 5-2 kwenye mchezo wa kwanza wiki iliyopita nchini Ubelgiji, Samatta akifunga mabao matatu peke yake.
Genk iliuanza vizuri mchezo wa leo ikipata mabao mawili ndani ya nusu saa, wafungaji kiungo wa Ukraine, Ruslan Malinovskiy dakika ya 14 na mshambuliaji Mkongo, Dieumerci N'Dongala dakika ya 32.
Lakini wenyeji wakazinduka na kusawazisha mabao yote hayo ndani ya saa moja ya mchezo, kupitia kwa mshambuliaji Mpoland, Kamil Wilczek dakika ya 34 na beki Msweden, Johan Larsson dakika ya 58.
Genk ikapata tena uhai na kufanikiwa kuongeza mabao mawili, la tatu akifunga beki Mbelgiji, Sebastien Dewaest dakika ya 66 na la nne Samatta dakika ya 87.
Chapisha Maoni