0
Kipa wa Youthe Rostand amekubaliana na Yanga kuondoka kikosini akiwa na uhakika wa kuvuna Sh 25 milioni, lakini katika kumalizia kikao hicho aliwaachia ujumbe mzito mabosi wa timu hiyo akiwaokoa wenzake watatu wanaosalia Jangwani.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga, zinasema kuwa, Rostand ambaye huenda tizi lake la jana Jumatano likawa la mwisho Jangwani, amewaambia mabosi wa timu hiyo kama wanataka makipa wenzake wasizomewe basi wabadilishe kocha wa makipa.
Bosi mmoja wa Yanga alisema Rostand amewaambia kupoteza kwake hali ya kujiamini kumetokana na Yanga kutokuwa na kocha bora wa makipa kitu ambacho hata Benno Kakolanya, Klaus Kindoki na Ramadhan Kabwili watakutana nacho.
Kipa huyo amewataka Yanga kutafuta kocha mpya wa makipa mwenye ubora ambapo amekuwa akiteseka katika timu hiyo kwa kuvumilia kwa muda mrefu na kwamba hana kinyongo katika kuondoka kwake.
“Tumemalizana na Rostand, lakini ametuachia ujumbe mzito ambao hata makocha mbalimbali wamekuwa wakituambia kwamba tunatakiwa kutafuta kocha wa makipa haraka,” alisema bosi huyo.
“Unajua amekuwa wazi kwamba hatuna kocha bora wa makipa na hata kama tutamuondoa lakini bado hatutakuwa hatujatibu tatizo la msingi.”
Anachota sh 25 milioni
Kuondoka kwa Rostand takwimu zinaonyesha atazoa kiasi cha sh 25 milioni kulingana na mkataba wake na Yanga ambao alisaini msimu mmoja uliopita.
Kipa huyo aliyekuwa akilipwa kiasi cha dola 1200 (sh 2.7 milioni) atajizolea kiasi cha dola 3600 (sh 8.1 milioni) ikiwa ni mishahara yake ya miezi mitatu anayodai.
Mbali na kiasi hicho pia kipa huyo atachukua kiasi cha dola 7500 (sh 17 milioni) ambacho ni kipengele cha kuvunja mkataba wake na kumfanya kuvuna jumla ya dola 11,100 (sh 25 milioni).
Zahera ajilipua mazima
Katika hatua nyingine Kocha, Mwinyi Zahera amewaambia mabosi wa Yanga kama wataiingiza timu hiyo kambini kwa wiki mbili tu basi kama akipoteza kizembe kama ilivyokuwa kwa Gor Mahia basi alaumiwe yeye na haraka kambi ikaandaliwa.
Kauli hiyo Zahera imekuja baada ya kushtukia wachezaji wake kutotunza mazoezi yao sambamba na kutokuwa sawa kisaikolojia.
Akizungumza na Mwanaspoti Zahera alisema amewataka mabosi wa klabu hiyo haraka kumtafutia kambi ya wiki mbili itakayorudisha ubora wa timu hiyo.
Zahera amesema Yanga inapokuwa hapa jijini Dar kumekuwa na mazingira ya wachezaji kutozingatia miili yao kupumzika na ameomba kambi ya haraka.
“Unajua hapa hatuwezi kuwa bora nimewaambia kwamba watafute kambi ya haraka tuondoke wachezaji wanafanya mazoezi makali lakini hujui kama wanajitunza namna gani huko wanakokwenda,” alisema Zahera.
“Kama tukiwa kambini tunaweza kuwa na ratiba ya mazoezi mara mbili kwa siku tukifanya asubihi na jioni lakini huko wachezaji watapumzika hakutakwa na kwenda kumuona mjomba wala dada pia watakuwa vizuri timu itaimarika.”
Kulifanyia kazi hilo vigogo wa kamati ya mashindano jana walikuwa wanahaha kuhakikisha timu hiyo inaelekea kambini mkoani Morogoro ambapo watakaa huko kwa wiki mbili wakijifua.

Chapisha Maoni

 
Top