Taifa Stars imejiweka pazuri katika Kundi L, baada ya kulazimisha suluhu ugenini dhidi ya Uganda iliyocheza mbele ya maelfu ya mashabiki wake waliojitokeza kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole jijini Kampala.
Matokeo hayo yanaifanya Taifa Stars kupanda hadi nafasi ya pili ikiwa na pointi mbili wakati Uganda ikijikita kileleni kwa pointi 4, kabla ya mchezo wa kesho wa Kundi L kati ya Cape Verde na Lesotho.
Kocha wa Stars, Emmanuel Amunike mbinu zake za kujilinda na kushambulia kwa kushtukiza zilizaa matunda jambo lililowapa wakati mgumu Waganda katika mchezo huo.
Katika mchezo huo wachezaji wa Taifa Stars wakiongozwa na nahodha, Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na Simon Msuva walishindwa kabisa kuonyesha uwezo kutokana na mvua na utelezi iliyowafanya washindwe kucheza vizuri.
Nahodha Samatta atajilaumu mwenyewe kwa kukosa bao la wazi katika kipindi cha pili akiwa yeye na kipa wa Uganda, Dennis Onyango na kutoka nje.
Mbali na ushambuliaji, safu ya ulinzi iliyokuwa na Abdi Banda, Aggrey Morris na Hamis Ramadhan Kessy walicheza kama wenyeji na kuzima mashambulizi ya Uganda yaliyotengenezwa na Emmanuel Okwi na Joseph Ochaya.
Hali ya mchezo ilivyokuwa kuanzia kipindi cha pili Stars walianza kwa kushambulia dakika 48, Gadie Michael alipiga shuti kali na kupanguliwa na Denis Onyango na kuwa kona ambayo haikuleta madhara kwa Uganda.
Hali ya hewa ilibadilika kwa kutoka jua kidogo, hali hiyo ilianza kuwaruhusu timu zote zicheze mpira wa chini kama ambavyo ilikuwa katika kipindi cha kwanza.
Dakika 56 Msuva alifanyiwa madhambi faulo ilipigwa Samatta, mpira ambao ulitaka kubadilisha ubao wa matokeo lakini hata hivyo ulienda pembeni.
Hali ya uwanja kukauka kutokana na jua kuwaka, kulifanya timu zote mbili kucheza soka la kutulia kwa kuanzisha mashambulizi kuanzia chini tofauti na kipindi cha kwanza walikuwa wakicheza pasi za juu.
Uganda walifanya mabadiliko kwa kumtoa Joseph Ochaya na kuingia Patrick Kaddu ili kuongeza nguvu katiika upande wa ushambuliaji ambapo ulionekana kupungua kasi baada ya Emmanuel Okwi kudhibitiwa vilivyo na mabeki wa Stars.
Dakika 70 Samatta alikosa goli la wazi baada ya kumchambua Denis Onyango (Kipa), lakini hesabu zaker zilikataa baada ya kurejesha mpira nyuma kwa kuchopu na kuikosesha Stars bao la kuongeza.
Stars walifanya mabadiliko kwa kumtoa Gadiel Michael na kuingia Farid Mussa, lengo likiwa ni kuongeza kasi katika eneo la ushambuliaji ambalo lilikuwa na kosa kosa nyingi.
Dakika 74 Msuva aliweza kukontroo mpira vizuri na kupiga krosi ndani ya kumi na nane na kukutana na Thomas Ulimwengu ambapo alikosea hesabu zake katika kufunga na mpira kuwa kona.
Stars walifanya mabadiliko dakika 78 kwa kumtoa Frank Domayo na kuingia Himid Mao, mabadiliko ambayo yalikuwa kwenda kuongeza nguvu katika safu ya kiungo, wakati huo Uganda nao walifanya mabadiliko kwa kumtoa Emmanuel Okwi na kuingia Luwaga Kizito.
Mpira uligeuka kuwa wa mabavu baada ya mabeki wa Uganda na washambuliaji wa Tanzania kucheza kwa kutoshana nguvu muda wote, ambapo Uganda walikuwa wakizuia huku Stars wakitafuta angalau goli la ugenini.
Uganda walifanya mabadiliko mengine dakika 87 kwa kumtoa Faruk Miya na kumuingiza Lubega Edrisa katika safu ya ushambuliaji, lakini hata hivyo mabeki wa Stars walikuwa makini mno.
Katika kipindi cha kwanza kulikuwa hakuna ufundi katika mchezo huu kutokana na mvua kuharibu uwanja hali iliyowafanya timu zote kucheza kwa kutumia mipira ya juu.
Stars iliwabidi wacheze kwa kuzuia sana kuliko kushambulia, lakini Uganda ambao walikuwa wakicheza kwa kushambulia nao walikuwa wanashindwa kutumia nafasi ambazo walikuwa wanatengeneza.
Mfumo wa 3-4- uliotumiwa na Stars ulikuwa wenye manufaa kwa upande wao kwani walikuwa na uwezo wa kukaba na kushambulia kwa wakati mmoja.
Maelewano ya mabeki Aggrey Morris, David Mwantika na Abdi Banda, yalikuwa na tija katika kikosi cha Stars kwani waliweza kumdhibiti mshambuliaji hatari wa Uganda, Emmanuel Okwi.
Katika kipindi cha pili timu zote zilibadilika na kucheza mpira wa chini wa kushambuliana, huku Uganda wakionekana kutumia miili yao vizuri katika kupambana na Stars.
Uwezo wa upambanaji kwa Thomas Ulimwengu, ulikuwa ukiisaidia Stars ambapo alikuwa akijitahidi kukaa na mipira licha ya kwamba muda mwingine alikuwa anasimama juu peke yake.
Katika upande wa kiungo, viungo Mudathir Yahya na Frank Domayo walikuwa na maelewano ya juu kwani walikuwa wanakaba na kushambulia kwa wakati mmoja.
Kikosi cha Stars : Aishi Manula, Kessy Ramadhani, Gadiel Michael/ Farid Mussa, David Mwantika, Aggrey Morris, Abdi Banda, Frank Domayo/ Himid Mao, Mudathir Yahya, Thomas Ulimwengu/ Shabaan Chilunda, Mbwana Samatta na Simon Msuva.
Chapisha Maoni